Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Dkt. Asha-Rose Migiro anakwenda kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Peter Kalaghe ambaye amerudishwa nyumbani.
Dkt. Asha-Rose Migiro ataapishwa kesho Alhamisi tarehe 05 Mei, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Gerson MsigwaKaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULUDodoma04 Mei, 2016-------------------------------
Mapito ya Dk. MigiroDk. Migiro alizaliwa tarehe 9 Julai 1956 katika Wilaya ya Songea, Ruvuma. Alisoma Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam mwaka 1963 hadi mwaka 1966.
Dk. Migiro alihamia Shule ya Msingi Korogwe, Tanga ambapo aliendela na elimu ya msingi mwaka 1967–1969.
Baadaye akajiunga kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Weruweru, Kilimanjaro mwaka 1970 hadi 1973 na Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Korogwe mwaka 1974 -1975.
Dk. Migiro alikuwa mmoja wa wasichana waliofaulu vizuri Korogwe Sekondari na alipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1977, alichukua masomo ya sheria na kuhitimu Shahada yake (LLB) mwaka 1980.
Baadaye aliajiriwa UDSM kufundisha masomo ya sheria kama Mhadhiri Msaidizi. Alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili kabla ya kuendelea tena na masomo ya juu ya sheria mwaka 1982–1984 hapohapo UDSM na kutunukiwa shahada ya uzamili (LLM).
Kati ya mwaka 1985–1988, alifundisha UDSM. Mwaka 1988 alikwenda Chuo Kikuu cha Konstanz, Ujerumani ambako alisoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika masuala ya Sheria mwaka 1992.
Dk. Migiro alirejea Tanzania akiwa Mhadhiri Mwandamizi na aliendelea kufundisha katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa.
Akiwa UDSM kati ya mwaka 1992 – 1994 Dk. Migiro alikuwa Mkuu wa Idara ya Sheria za Katiba na Utawala.
Kati ya mwaka 1994 – 1997 aliongoza Idara ya Sheria za Makosa ya Jinai (Idara zote zipo katika Kitivo cha Sheria UDSM).
Dk Migiro ni mzungumzaji mzuri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani. Ni mke wa Profesa Cleophas Migiro na wana watoto wawili wa kike.
Dk Migiro alianza na siasa za kujijenga akitokea katika taaluma. Mwaka 2000, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa waziri kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto.
Alitumikia wadhifa huo hadi mwaka 2005 bila kubadilishwa akisimamia mambo mengi ya kisera na kimiundombinu, bila kusahau utekelezaji na upiganiaji wa haki za wanawake na watoto.
Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, alimteua kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje, Januari 2006 na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa huo. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, alifanya kazi nyingi za kimataifa zilizomweka katika anga nyingine kisiasa.
Januari 5, 2007, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu (UN) mpaka 2012 alipomaliza muda wake. Januari mwaka 2013, Dk Migiro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Desemba 2013 aliteuliwa kuwa mbunge katika Bunge la Tanzania.
Januari 2014 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, nafasi ambayo alidumu nayo mpaka Rais Kikwete alipomaliza muda wake mwaka jana
Article Source: Mwanaharakati Mzalendo
Comments