Shaaban nditti anamaliza msimu wake wa 17 mfululizo katika ligi kuu
Tanzania bara na mchezaji huyo wa zamani wa Taifa Stars bado ana nguvu,
maarifa, mbinu, na uwezo wa kupambana bila kuchoka na wachezaji vijana.
Wakati wengi ‘wameingia na kutoka’ katika ligi kuu bara, Nditti
amedumu tangu mwaka 1999 alikoanza soka lake akiwa na timu ya Singida
United ya Singida. Alisajiliwa na Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza mara
baada ya Mtibwa kutwaa ubingwa wao wa pili mfululizo wa VPL mwishoni mwa
2000.
“Na bado kama Mungu anampa uzima basi atafikisha miaka 25 maana bado
mwenye nguvu na anawajibika ipasavyo, na pia ana jitunza haswa”, anasema
Yusuph Mgwao mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na Mtibwa ambaye
amewahi kucheza na Nditti katika timu zote hizo miaka ya 2004 na 2005.
Nditti aliondoka Mtibwa na kusajiliwa na Simba mwishoni mwa mwaka
2003 lakini alishindwa kutulia klabuni hapo na baada ya kumalizika kwa
msimu wa 2004 akaamua kurejea Mtibwa ambako amedumu kwa miaka 12
mfululizo bila kuhama huku akitumia misimu miwili tu kati ya 17 kucheza
nje ya timu hiyo ya Turiani, Morogoro.
Akiwa mshindi wa taji la ligi kuu mwaka 2004 akiwa na Simba, Nditti
ameichezea timu ya Taifa kwa miaka zaidi ya kumi na kila kocha wa kigeni
kuanzia, Mbrazil, Marcio Maximo (2006 hadi 2010,) Wadenish JAN na KIM
Poulsen wote walipendezwa na nidhamu ya Nditti, mchezo wake wa uhakika
akiwa katikati ya uwanja.
“Namkubali sana ‘ankol’ na najivunia sana kuwahi kucheza naye timu
moja. Mwenyezi Mungu amlinde naamini atazidi kucheza kwa miala mingi
zaidi sababu anatumia sana akili kuliko nguvu. Heshima kubwa sana
kwake.” anasema mshambulizi Juma Ndanda Liuzio ambaye sasa anakipiga
katika timu ya Zesco United ya Zambia.
Liuzio ni mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Mtibwa kisha ile ya
wa kubwa alicheza na Nditti kwa misimu miwili klabuni Mtibwa. “Nidhamu
yake nje na ndani ya uwanja ndiyo silaha yake kubwa, nilimpokea kwa mara
ya kwanza akiwa kijana mdogo pale Singida. Mungu amsimamie ‘my young
brother’ Nditti.” ni maneno ya mlinzi wa zamani wa Yanga SC, Mzee
Abdallah.
Nilimtafuta msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru na kutaka kufahamu kama wataendelea kuwa Nditti msimu ujao.
“Amekuwa kiongozi mzuri kwa wachezaji ndani na hata nje ya uwanja.
Amekuwa hapa kwa miaka zaidi ya 14, hapa ni nyumbani kwake na sisi kama
Mtibwa tunafarijika kumuona akicheza katika kiwango cha juu kila msimu.
Bado tunahitaji huduma na ya kapteni wetu Nditti lakini kwa sasa siwezi
kusema zaidi, ila Nditti atabaki Mtibwa na tutakuwa nae msimu ujao”,
anasema Kifaru.Inatoka kwa mdau.
Comments