Na Baraka Mbolembole
Mshambuliazi wa kimataifa raia wa Burundi, Amis Tambwe amefanikiwa
kuvunja rekodi yake mwenyewe ya magoli katika historia ya wachezaji wa
kulipwa katika ligi kuu Tanzania bara (VPL).
Mrundi huyo kwa mara ya kwanza alitua Tanzania na kujiunga na Simba
SC akitokea Vitalo’O ya kwao Burundi msimu wa 2013/14 na kufanikiwa
kushinda tuzo binafsi ya mfungaji bora baada ya kufunga jumla ya magoli
19.
Awali kabla ya ujio wa Tambwe mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya,
Boniface Ambani alikuwa akishikilia rekodi ya mfungaji wa magoli mengi
zaidi kwa msimu kwa wachezaji wa kigeni, si hivyo tu, Ambani aliweka
rekodi ya mshambulizi aliyefunga magoli mengi zaidi (17) akicheza msimu
wake wa kwanza VPL.
Lakini huyu Tambwe ‘Mr. hat-trick’ ni balaa. Ni mfano bora zaidi wa
kulipwa na bila shaka vijana wengi washambuliaji wa baadaye watakuwa
wakijifunza namna mchezaji huyo alivyo stadi kiufungaji. Utulivu wake,
ufuatiliaji wake wa ‘move’ za mchezo, uwezo wake wa kujipanga, kutumia
nafasi, kujitengenezea nafasi yeye mwenyewe na kutengeneza nafasi za
kufunga kwa wachezaji wenzake.
Tambwe alifunga jumla ya magoli 15 msimu uliopita akichezea Simba
hadi nusu ya msimu kisha kujiunga na Yanga baada ya kutemwa na timu yake
hiyo ya kwanza Tanzania kwa madai ya kuporomoka kwa kiwango chake chini
ya mkufunzi Mzambia, Patrick Phiri.
Yanga ilifanya usajili wa Tambwe muda mfupi baada ya kumtimua
aliyekuwa kocha wao Mbrazil, Marcio Maximo mwezi Disemba, 2014. Chini ya
Mholland. Hans Van der Pluijm, Tambwe amefanikiwa kufunga jumla ya
magoli 35 katika VPL pekee katika kipindi cha miezi 14 waliyofanya kazi
pamoja klabuni Yanga.
Jumanne hii, Mrundi huyo amefanikiwa kufunga goli lake la 20 msimu
huu huku zikiwa zimesalia game nne kabla ya kumalizika kwa msimu. Tambwe
ni mtulivu licha ya siku za karibuni baadhi ya watu kudai kwamba
kiwango chake kimeshuka jambo ambolo si la kweli.
“Nina cheza vizuri na kuisaidia timu yangu kupata ushindi. Watu
wanataka kuniona nikifunga kila mara na inapotokea sifungi wanasema
nimeshuka kiwango. Wanatakiwa kutazama na mchango wangu kwa wachezaji
wengine, si lazima nifunge mimi lakini nachukia kumaliza mechi bila
kufunga”.
Anasema mshambulizi huyo wakati nilipofanya nae mahojiano mafupi kwa
njia ya mtandao baada ya kufunga goli lake la 20 msimu huu na kuisaidia
Yanga kushinda 3-1 ugenini dhidi ya Stand United katika game ambayo
ilishuhudiwa mshambulizi-pacha wake, Donald Ngoma akizamisha magoli
mawili, goli moja kwa usaidizi wa Tambwe.
Goli lake hilo limemfanya kumpiku mshambulizi Mganda, Hamis Kizza
ambaye hadi kufikia mchezo wa 22 wa timu yake ya Simba alikuwa amefunga
magoli 19 ambayo amesimamia hapo hadi sasa. Wakati timu yake ikihitaji
pointi tatu tu baada ya game ya Azam FC siku ya Jumatano, Tambwe
amefunga magoli 20 kati ya 61 ya timu yake ambayo katika michezo 26 ya
msimu uliopita ilifanikiwa kufunga jumla ya magoli 52 kwa msimu wote.
Yanga imefunga jumla ya magoli 61 katika michezo 26 ya msimu huu (magoli
9 zaidi ya msimu uliopita).
Wakati msimu uliopita katika ligi iliyokuwa na michezo 26, Yanga
waliruhusu nyavu zao mara 18 msimu huu wamepelekwa nyavuni mara 15
(magoli matatu pungufu ya yale ya msimu uliopita.
Bila shaka ubingwa utaenda tena Yanga msimu huu, na Tambwe atatetea
tuzo binafsi ya ufungaji bora ambayo alishuhudia ikienda kwa mchezaji
mwenzake wa Yanga, Saimon Msuva msimu uliopita baada ya kufunga jumla ya
magoli 17 (magoli mawili zaidi yake).
Tambwe amefunga jumla ya magoli 54 katika msimu wake wa tatu VPL.
Hakuna mkali wa nyavu kama Mrundi huyu. Mfalme wa magoli ya kichwa.INtoka kwa Shaffih Dauda
Comments