Cuba imesema itaendelea kuwa mshirika wa karibu zaidi na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa ujumla katika harakati za kukuza uchumi
Na Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewasili Mjini Havana Nchini Cuba kuendelea na ziara yake ya Kiserikali akitokea Nchini Israel.
Balozi Seif na Ujumbe wake amepokewa na Naibu Waziri wa Mamo ya Nchi za Nje wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Marcos Rodrigues Costa pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania Walioko Nchini humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi ameambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri Ofisi ya Waziri Kiongozi Mh. Mohd Aboud Mohd, Waziri wa Afya Mh. Juma Duni haji, Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dr. Malik Abdulla Juma pamoja na baadhi ya Maafisa wa Serikali.
Balozi Seif na Ujumbe wake amekutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamuhuri ya Cuba Bwana Esteban Lazo Hernandez yaliyofanyika katika Jumba la Mapinduzi Mjini Havana.
Bwana Esteban alisema Cuba itaendelea kuwa mshirika wa karibu na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika harakati za kuwaletea Maendeleo na ustawi wa Jamii Wananchi wa pande hizo mbili.
Bwana Esteban alifahamisha kwamba Mipango itazidi kuimarishwa ili kuona uhusiano wa Kihistoria wa sehemu hizo mbili unakuwa wa kudumu.
Aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwa kuendeleza amani na Demokrasia ambayo ni kielelezo cha kuigwa na Mataifa mengi Duniani na hasa yale ya Bara la Afrika.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Cuba kwa moyo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kuimarisha Utawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema Msaada wa Cuba kwa Zanzibar umekucha chachu ya kuondokana na matatizo mbali mbali ya Jamii hasa yale ya Sekta ya Afya.
Hana hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Visiwa vya Zanzibar viko mlango wazi katika kuwakaribisha wawekezaji wa Cuba kuwekeza Vitega Uchumi vyao ili kusaidia kunyanyua Uchumi wa Taifa.
Comments