Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho, Peter Kisumo |
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama ameonywa akitakiwa kubadilika kwa sababu amekuwa mzigo.
Taarifa kutoka ndani ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), zilieleza kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho, Peter Kisumo ndiye alikuwa mchokozaji ambaye bila kumung’unya maneno alisema Mukama ameonyesha utendaji mbovu tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Akijadili hali ya kisiasa nchini, Kisumo anadaiwa kumtuhumu Mukama kutumia muda mwingi kusema misamiati isiyokuwa na maana na faida kwa CCM.
“Unajua mzee (Peter Kisumo) alichana siyo kawaida, alimwambia Katibu kuwa ameshindwa kumaliza makundi, lakini amekuwa ni bingwa wa misamiati ambayo haina maana, amemwambia asipokuwa makini chama kinakwenda pabaya,” kilieleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati Kisumo akishusha shutuma hizo, makofi mengi yalikuwa yakipigwa kuashiria kuungwa mkono na wajumbe wengi, lakini Mukama hakujibu chochote.
Pia, Mukama anadaiwa kushindwa kusimamia mikakati ya chama na makatibu wa CCM wakidaiwa kuwa wamekuwa dhaifu na hawana mipango mikakati ya kupambana na upinzani.
Kisumo alidai kuwa Mukama ameshindwa kuonyesha kama chama kinapanda kwenye duru za chini, huku akipendekeza pande zote zinazohasimiana ndani ya CCM kukaa pamoja na kuondoa tofauti zao ili kukinusuru.
Comments