ALIYEKUWA mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema kuwa kitendo cha
klabu yake kufanikiwa kumnasa, Paschal Wawa ni sawa na kulipiza kisasi
kwa watani zao Yanga ambao pia walikuwa wanamwania beki huyo wa kati
kutoka Ivory Coast.
Wawa alitua Simba mapema wiki hii lakini bado hajasaini mkataba baada ya
kupewa masharti ya kuonyesha kiwango cha juu katika mashindano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame yanayoanza leo
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza , Rage alisema kuwa amejisikia faraja sana kuona Simba
imewazidi "kete" Yanga katika mbio za kumsajili Wawa ambaye aliwahi
kuitumikia Azam FC misimu miwili iliyopita.
Rage aliitakia mafanikio zaidi Kamati ya Usajili ya Wekundu wa Msimbazi
kuwapata nyota wote inaowahitaji ili waweze kufanikiwa zaidi katika
msimu ujao.
"Hii ndio furaha yetu, kuifanya Yanga ipepesuke na iwe dhaifu, nakumbuka
walinidhalilisha sana wakati wa usajili wa Mbuyu Twite, sasa nasisi
tumelipiza kisasi, na bado, kama kuna mchezaji mwingine wanamtaka
nawaomba viongozi wangu wamsajili," alisema Rage.
Aliongeza kuwa Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa na ushindani zaidi hivyo
ni lazima kila upande unatakiwa kujiimarisha kwa lengo la kujiandaa
kufanya vizuri katika msimu ujao.
"Simba pia mwakani inashiriki mashindano ya kimataifa, lazima tuwe imara
kila idara kwa sababu tunataka kufika mbali," alisema katibu mkuu huyo
wa zamani wa Chama cha Soka Tanzanai (FAT sasa TFF).
Kwa sasa Simba inajiandaa kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame ikiwa
imepangwa kuanza kampeni za kuwania ubingwa wa michuano hiyo kesho kwa
kucheza na Dakadaha ya Somalia.
Comments