Mkazi wa Mtaa wa Mamboleo B wilayani Temeke, Joseph Liapinda (84) amemsifu na kusimulia jinsi aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, ambaye kwa sasa ni Mbunge Muleba Kusini mkoani Kagera (CCM), Profesa Anna Tibaijuka alivyomsaidia kuokoa nyumba yake iliyotaka kudhulumiwa.
Profesa Anna Tibaijuka
Kauli imetolewa leo jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Karimjee alipokutana na Profesa Tibaijuka katika kuuaga Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini mkoani Tanga,Stephen Ngonyani ‘Profesa Maji Marefu’ (CCM).
Liapinda amesema mwaka 2014 nyumba yake iliyoko Kata ya Sandali wilayani humo ilitaka kudhulumiwa na mtu aliyemruhusu kukaa bure kwa makubaliano ya kujenga choo akishirikiana na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo.
Amebainisha kuwa mtu aliyekuwa akikaa kwenye nyumba yake hakujenga choo na mwenyekiti wa mtaa huo akishirikiana na mjumbe wa nyumba kumi, Josephina Francis walimpa namba feki ya nyumba iliyomwekeza kuwa sio yake.
Amesisitiza kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho alianza kupigania haki yake kwa kwenda Makao makuu ya wizara husika ndipo alipokutana na Profesa Tibaijuka na kumueleza mkasa mzima ambapo Mbunge huyo alimpa barua yenye maelekezo iliyomtaka aende kwa aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Galawa.
Amefafanua kuwa baada ya kwenda kwa mkuu wa wilaya huyo na kwamba yule aliekuwa amempa hifadhi katika nyumba yake alikamatwa na kuwekwa ndani na kurudishiwa nyumba hiyo katika himaya yake.
Amemshukuru Profesa Tibaijuka kwa kusema bila msaada wake nyumba yake asingeipata na kwamba anaishi na familia yake ya watoto sita pamoja na mkewe.
Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka amempa shukrani mkazi huyo kwa kutambua mchango wake uliofanikisha kuokoa nyumba yake kwa wadhulumati na kumsisitiza aendelee kuishi kwa amani.
Katika hatua nyingine, Profesa Tibaijuka amesema ameupokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Maji Marefu kwa kuwa alikuwa ni mtu msikivu, mwelewa na mjenga hoja bungeni.
“ Ni masikitiko makubwa Maji Marefu namfahamu alikuwa mbunge mwelewa na mjenga hoja tulipokuwa bungeni, “ amesema.
Comments