SERIKALI
imesitisha ongezeko la tozo zilizoanza kutumika hivi karibuni katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo ndiyo yenye vifaatiba na
madaktari wenye uwezo mkubwa kuliko hospitali yoyote nchini.
Hatua
hiyo ya Serikali, ipo katika kauli ya Serikali bungeni, iliyotolewa jana
na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, ambapo pia Bohari
ya Dawa (MSD) iliagizwa kupeleka dawa muhimu zenye thamani ya Sh
milioni 200 katika hospitali hiyo.
Hivi
karibuni hospitali hiyo ilipandisha gharama za huduma hospitalini hapo,
ambapo mgonjwa aliyetakiwa kulazwa baada ya kupatiwa rufaa kutibiwa
katika hospitali hiyo, alipaswa kulipa Sh 5,000 kwa siku na Sh 2,000 za
chakula, ambazo hazikuwepo hapo awali.
Taarifa
ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, , ilikaririwa na vyombo vya
habari, ikieleza kuwa gharama mpya zilianza kutumika Oktoba 17, mwaka
huu.
Kutokana
na gharama hizo, baadhi ya wahudumu hospitalini hapo walikaririwa
wakisema idadi ya wagonjwa imepungua wodini kutokana na wengi wao
kushindwa kumudu gharama.
Wagonjwa kutoka mikoani waliathirika zaidi, kwa kulazimika kutafuta malazi nje ya hospitali hiyo, hata kama hali zao ni mbaya.
Aidha,
baadhi ya wananchi waliokuwa wakiuguza ndugu zao, walikaririwa kuchukua
uamuzi wa kuwarejesha nyumbani ili kukwepa gharama hizo.
Miundombinu
Mbali na
kusitisha ongezeko hilo la tozo, Dk Seif pia ameagiza uongozi wa
hospitali hiyo kurekebisha mara moja mazingira na miundombinu ya
hospitali hiyo, ambayo yapo ndani ya uwezo wao.
Ingawa
tamko hilo halikufafanua, lakini taarifa zinaonesha kuwa hospitali hiyo
ilikuwa ikizidiwa na wagonjwa, kiasi cha baadhi kulazimika kulala
sakafuni.
Vyombo
vya habari viliripoti kuhusu hali ya usafi wa vyoo vya wodi ya Sewa Haji
kuwa mbaya, licha ya kuwapo taarifa za kutolewa kwa zabuni kwa kampuni
kadhaa kufanya usafi, unaokidhi viwango na kanuni za afya bora.
Baadhi ya vyoo havikuwa na maji na vifaa vya kusukuma maji havikuwa vikifanya kazi, huku baadhi ya mabomba yakiwa na kutu.
Kutokana
na ukosefu wa maji, wagonjwa na watu wanaowatembelea, alilazimika
kutumia maji yaliyopo kwenye mapipa nje ya vyoo na yalipokosekana,
walitafuta mahali kwingine ikiwamo nje ya jengo hilo.
Baadhi ya
vyombo vya habari, viliripoti kushuhudia baadhi ya vyoo vikiwa vimejaa
uchafu katika majengo ya Sewa Haji, Kibasila na Mwaisela huku vingi
vikiwa katika hali mbaya ya uchakavu, kutokana na kutumika muda mrefu
bila kufanyiwa ukarabati.
Deni MSD
Kuhusu
deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Dk Rashid alisema Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha ilifanya uhakiki wa
deni la MSD la Sh bilioni 41.5.
Baada ya
deni hilo kuhakikiwa, alisema Serikali ilianza kulipa kwa awamu ambapo
Sh bilioni 8 zililipwa Juni 14, Sh bilioni 2 Agosti na Sh bilioni 20
zimelipwa mwezi huu. Alisema kiasi kilichobaki cha Sh bilioni 11.5,
kitalipwa mwezi ujao.
Kuhusu
kutenga fedha za kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kupitia
MSD ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata dawa na vifaa tiba kwa
wakati, alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Bunge liliidhinisha
Sh bilioni 70.5 kwa ajili ya kazi hiyo. Ocean Road Akizungumzia huduma
za afya katika Hospitali ya Ocean Road, alisema huduma za matibabu ya
saratani inaendelea kutolewa,
kutokana na mashine ya E80 kuendelea kufanya kazi na kwa sasa ndiyo inayotibu wagonjwa wote wa saratani katika taasisi hiyo.
"Kutokana
na kuwepo kwa mashine moja tu ya mionzi inayofanya kazi, kwa sasa hivi
mashine inafanya kazi kwa saa 18 kwa siku ili kupunguza mlundikano wa
wagonjwa.
"Mashine
ya intra cavitary ambayo ilikuwa imesimama kufanya kazi kutokana na
ubovu na kukosekana kwa vifaa muhimu, imetengenezwa na sasa imeanza
kufanya kazi hivyo kuwezesha matibabu ya wagonjwa wa saratani ya shingo
ya kizazi kwa ufanisi zaidi," alisema Waziri.
Nafasi ya Njelekela yatangazwa
Wakati
hali ikiwa hivyo, nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili,
ilitangazwa jana kuwa iko wazi. Sifa za mtu anayetakiwa kujaza nafasi
hiyo ni pamoja na Shahada ya Uzamili katika Udaktari wa Binadamu; au
sifa inayolingana na hiyo katika masuala ya udaktari na upasuaji, pamoja
na uzoefu wa zaidi ya miaka kumi katika uongozi wa hospitali.
Tangazo
hilo lilitolewa na hospitali hiyo na lilikuwa katika gazeti la Daily
News la jana, Ukurasa wa Nne. Waombaji wenye vigezo vinavyotakiwa,
wanatakiwa watume maombi ya kazi hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa Hospitali.CHANZO:BONGO LEAKS
Comments