Washington. Ujumbe wa Tanzania katika mikutano muhimu inayofanyika Marekani wameipigia debe nchi yao wakitaka ikumbukwe.
Katika mkutano wa 45 wa Kamisheni ya
Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UN) na mkutano wa wazi wa tisa wa kikosi
kazi kuhusu mapendekezo ya ajenda za malengo mpya ya maendeleo endelevu
baada ya 2015 (SDGs), wamekuwa wakitetea masilahi ya nchi kwa kushiriki
na kuchangia majadiliano ya mada mbalimbali zinazohusiana na mikutano
hiyo
.
Akichangia katika mada iliyohusu
Technolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa alisema mwaka hadi mwaka Tanzania na
Afrika imeendelea kupiga hatua katika teknolojia ya habari na
mawasiliano licha ya changamoto mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo
kuwa ni kutokuwapo kwa uratibu kati ya wazalishaji wa takwimu za ICT na
watumiaji na kati ya wazalishaji na watoaji wa takwimu ambao ni chanzo
muhimu cha taarifa.
Alisema tatizo hili kama
halitarekebishwa, linaweza kusababisha uchapishaji usio sahihi wa
takwimu kuhusu ICT, jambo ambalo linaweza kusababisha utoaji uamuzi
wenye makosa.
Alisema uboreshaji na uratibu kati ya
wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa takwimu, utaepusha kujirudia kwa
makosa yakiwamo ya matumizi ya rasilimali fedha na watu, rasilimali
ambazo ni haba katika Afrika.
''Kipengele cha takwimu za ICT
kinapaswa kuingizwa katika mikakati ya kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya
takwimu na katika mipango ya kazi ya kikanda, '' alisema.
Dk. Chuwa alisema ukusanywaji wa
takwimu katika ngazi za kitaifa lazima uimarishwe kwa kuweka utaratibu
kati ya taasisi husika pamoja na Ofisi za Taifa za Takwimu.
Kuhusu uwezeshaji, alisema Afrika
inahitaji kuimarisha uwezo wake wa kutafuta rasilimali ndani ya Afrika
ili hatimaye Afrika ijijengee uwezo wa kuboresha ukusanyaji, uchambuzi
na usambazaji wa viashiria vya msingi vya ICT katika Afrika.
Alisema Tanzania ingependa kuona
wataalamu walioandaa mfumo huo, wanakuja na mkakati wa utoaji mafunzo na
uwezeshaji kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania(E.L).source http://www.mjengwablog.com/
Comments