Na Hamdi Salad, Mogadishu
Serikali ya Somalia inakabiliwa na upinzani kutoka Ahlu Suna wal Jamaa
(ASWJ) baada ya pande hizo mbili kutokufikia makubaliano juu ya
kuviunganisha vikosi vyao kwenye kampeni ya kijeshi inayoendelea sasa
dhidi ya al-Shabaab mkoani Galgadud.
Wanajeshi wa Jeshi la Taifa la Somalia
(SNA) wakiwa wamekaa kwenye lori mjini Qoryooley baada ya operesheni
iliyofanikiwa kwenye Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia kuukomboa
mji huo kutoka kwa wanamgambo wa al-Shabaab siku ya tarehe 22 Machi
2014. [PICHA YA AFP / AU UN IST / TOBIN JONES]
Uhusiano kati ya serikali na wanamgambo hao wanaoshirikiana na serikali
yalianza kuzorota mwishoni mwa mwaka jana juu ya ahadi ambazo
hazikutekelezwa, naibu mwenyekiti wa kamati tendaji ya ASWJ, Sheikh
Ahmed Abdullahi Ilkaase, aliiambia Sabahi.
Wakati operesheni ya jeshi la serikali ilipokaribia kwenye maeneo
yanayodhibitiwa na ASWJ, serikali ilituma ujumbe mjini Dhusamareb, mji
mkuu wa mkoa wa Galgadud, mnamo tarehe 19 Machi kuwaomba ASWJ kupigana
chini ya Jeshi la Taifa la Somalia sambamba na Kikosi cha Umoja wa
Afrika nchini humo (AMISOM).
Lakini ujumbe huo, akiwemo Waziri wa Ulinzi Mohamed Sheikh Hassan Hamud,
Wazri wa Usalama wa Taifa Abdikarim Hussein Guled, Waziri wa Habari
Mustafa Ali Duhulow, na Waziri wa Mambo ya Ndani na Masuala ya
Shirikisho Abdullahi Godar Barre ulikumbana na upinzani kutoka upande wa
ASWJ, ambao unahisi ulikosewa kwenye makubaliano ya usalama yaliyopita.
"[Mawaziri hao] walitwambia tuachane na jina na uongozi wetu na
wapiganaji wetu wapigane chini ya serikali ingawa bado hawajatekeleza
makubaliano ya awali yaliyofikiwa Abudwaq kati yetu na serikali,"
Ilkaase alisema. "Kwa hivyo, tuliyakataa."
Comments