Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Salum Madadi kuwa Mkurugenzi wake mpya wa Ufundi.
Uteuzi huo umefanya na Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi, Madadi alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Januari mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Ufundi aliyekuwepo kumaliza mkataba wake Desemba 31 mwaka jana.
Madadi mwenye leseni A ya ukocha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni kocha mwenye uzoezi wa zaidi ya miaka 30 ambapo alianza kufundisha mpira wa miguu mwaka 1980 katika klabu ya Maji SC ya Lindi.
Ana elimu ya sekondari aliyoipata katika shule ya Chidya na diploma ya ukocha wa mpira wa miguu aliyoipata nchini Ujerumani. Pia ni Mkufunzi wa makocha wa CAF, na alijiunga na TFF mwaka 2006 akiwa Ofisa Maendeleo.
Alikuwa Kocha wa Taifa Stars mwaka 2000. Mbali ya Maji SC, amewahi kufundisha timu za Nyota Nyekundu, Ushirika ya Moshi, Simba, Shangani ya Zanzibar, Malindi ya Zanzibar, Cardif ya Mtwara na Kariakoo ya Lindi.
Pia amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Comments