Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba limepitisha kanuni ya kuwazuia waandishi
wa habari kuingia katika vikao vya kamati za chombo hicho, hatua ambayo
inaelezwa ni kinyume na Katiba inayotoa uhuru wa wananchi kupata
habari.
Mwenyekiti wa muda wa Bunge la katiba,Pandu kificho.PICHA|MAKTABA
Kanuni hiyo ilipitishwa jana baada ya malumbano makali yaliyowagawa
wajumbe wa bunge hilo, baadhi wakipinga kifungu hicho kwa sababu
kinavunja Katiba ya nchi inayotoa uhuru kwa waandishi kukusanya na
kusambaza habari na wengine wakiunga mkono kuwazuia.
Kanuni hiyo ilipitishwa kwa mbinde huku baadhi ya wajumbe wakiendelea
kushikilia msimamo wa kuikataa, hata baada ya Mwenyekiti wa Muda wa
bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kuridhia kipite. Wajumbe waliopinga
kanuni hiyo ni Joshua Nasari, Moses Machali, Peter Serukamba, Ezekiah
Wenje na Maria Sarungi.
Baadhi ya wajumbe akiwamo Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Kajubi Mukajanga walisimama kutaka kuzungumza lakini hawakupata
fursa hiyo.
Mjumbe aliyekuwa mwiba kwa Tasnia ya Habari ni, Dk Harrison Mwakyembe
ambaye aliwashawishi wajumbe kufunga mjadala huo ili wasonge mbele kwa
madai kuwa hata yeye pia ni mwanahabari. “Hakuna upande usiotambua
umuhimu wa vyombo vya habari katika mchakato huu... Tunachotofautiana ni
jinsi na namna
ya ushiriki wa vyombo vya habari,” alisema Dk Mwakyembe. Alisema Taifa
limeingia katika kipindi maalumu kama cha vita na kwa msingi huo, kanuni
zinabadilika kulingana na mazingira na kwamba vyombo vya habari
vinapaswa kulitambua hilo.
Hata hivyo, Kifungu cha 57 (3) katika kanuni hiyo kilipita baada ya
kufanyiwa marekebisho kuondoa maneno ‘mwenyekiti anaweza kutoa taarifa’
badala yake, ikawa ‘ni lazima kutoa taarifa.’
Kanuni hiyo inampa mamlaka mwenyekiti wa kamati au mjumbe yeyote kwa
idhini yake, kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mambo
yaliyojitokeza kwenye kikao.
Mjadala wakwama
Mvutano juu ya kifungu hicho ulianza juzi jioni wakati baadhi ya wajumbe walipotofautiana.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti, Mjumbe George
Simbachawene alisema iwapo waandishi wataruhusiwa wangeweza kutoa
taarifa zisizochujwa ambazo zitawachanganya wananchi.
Hata hivyo, Mjumbe wa bunge hilo, Ezekiah Oluoch alisema kisheria kanuni
hiyo ilikuwa inakwenda kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi ambayo
kimsingi, ndiyo sheria mama. Aliisoma ibara hiyo akisema kama wajumbe
wataruhusu kupitishwa kwa kifungu hicho, litakuwa kosa kubwa la kuvunja
katiba ya nchi.
Ibara hiyo ya 18 ya katiba inasomeka, “Kila mtu anayo haki ya kutafuta,
kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi… anayo haki ya kupewa
taarifa wakati wowote kuhusu matukio muhimu kwa maisha na shughuli za
wananchi, pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.”
“Hapa tuko kwa masuala muhimu kwa jamii kama waandishi wa habari wa
Tanzania wana matatizo katika kuripoti habari za Bunge, hilo ni tatizo
jingine, hatuwezi kutunga kanuni zinazokwenda kinyume na Katiba ambayo
ndiyo sheria mama,” alisema.
Akichangia hoja hiyo, Mjumbe Halima Mdee alisema: “Namshangaa Mheshimiwa
Simbachawane kwani yeye ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na
anajua kwamba waandishi wanaruhusiwa kwenye vikao vya kamati. Iweje hapa
kwenye Bunge la kutunga Katiba?
“Ninachokiona ni kwamba waandishi wa habari wanakatazwa kwa sababu ya
hofu. Hii siyo Katiba ya kikundi cha watu 629 tuliopo hapa. Hii ni
Katiba ya wananchi na wanayo haki ya kujua majadiliano yanayoendelea
katika Kamati.”
Mjumbe Machali alisisitiza kuwa kuwazuia waandishi ni kukiuka Katiba na
kuhoji: “Nyie mnaosema mnataka kura za wazi ili wananchi wajue, mnaogopa
nini? Katika hoja hiyo, Mjumbe Freeman Mbowe alisema Katiba ni mali ya
wananchi na kwamba wana haki ya kufahamu kila kinachoendelea ndani ya
Bunge.
“Kuna Watanzania kwa mamilioni ambao wanatusikiliza, kinachoonekana hapa
tunaanza kuweka mkakati wa kuchuja nini kipelekwe kwa wananchi na hii
ni hatari sana katika mchakato wa Katiba,” alisema.
Alisema vyombo vya habari vina umuhimu wa kuripoti kila kinachoendelea
ndani ya kamati na utaratibu wa kuwaruhusu waandishi wa habari kuripoti
katika kamati umetumika katika nchi za Kenya na Afrika Kusini.
Baada ya hoja hizo za juzi usiku, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa
Costa Mahalu alisema: “Wajumbe ndiyo mnaokubali au kukataa mapendekezo
yaliyotolewa na kamati yetu. Sisi mnatuagiza tunarekebisha mwafaka
uliofikiwa na wajumbe na kuonyesha msimamo wao kwa pamoja, naomba hili
tulirudishe kwa wajumbe wenyewe waliamue.”
Hata hivyo, malumbano zaidi yaliendelea jana na Mwenyekiti Kificho alitoa taarifa ya kukubaliana na mapendekezo ya kamati yake.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Comments