Mwandishi wetu-MAELEZO
Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa fursa kwa watu wengi kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi kwa mapana, katika Taasisi za serikali na Taasisi binafsi.
Akizungumza katika mjadala wa Clouds Media katika kipindi cha The Big Breakfast chenye kauli mbiu ya The power of Man yaani Nguvu ya Pamoja kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Serena, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi alisema kuwa serikali inaendelea na jukumu la ujenzi wa nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Tunatambua na kuheshimu nguvu ya wengi kama kauli mbiu hii inavyoeleza, katika dhana ya maendeleo kuna mengi Serikali inafanya ili kutekeleza azma yake kwa wananchi, mfano Ujenzi wa madaraja mbalimbali nchini, Miradi ya Maji, Miradi ya Umeme, Ujenzi wa vituo vya afya na Hospitali na kulete ndege, kwetu sisi haya ni maendeleo makubwa sana”, Dkt. Abbasi.
Katika dhana ya Nguvu ya pamoja, Dkt. Abbasi alisema kuwa kauli mbiu hii inaonesha namna gani sasa haya mambo ambayo Serikali inafanya yanawafikia wananchi na kuwanufaisha popote walipo.
Dkt.Abbasi alieleza kuwa katika mjadala wa nguvu ya pamoja dhana ya maendeleo ina nadharia mbili ambazo wasomi wanazijadili duniani kote ikiwa ni moja ya miongozo ya maenedeleo duniani, huku wakiamini katika nadharia ya maendeleo ni watu na wengine wakiamini katika nadharia ya maendelo ni vitu.
“nilichokisema ni kwamba duniani kuna mjadala mkubwa sana katika suala la maendeleo, wapo wanaoamini kwamba maendeleo ni watu kwa mambo yanafanyika moja kwa moja na yanagusa watu, wapo wanaoamini kwamba maendeleo ni vitu kwamba huwezi kuwaendeleza watu bila kuwajengea miundombinu kama vile barabara, reli, umeme na maji”, Dkt Abbasi.
Katika kuunga mkono kauli mbiu ya nguvu ya pamoja, Dkt Abbasi alieleza kuwa katika nadharia mbili za maendeleo Serikali inaamini katika nadharia zote yaani maendeleo ni vitu kwani inatekeleza miradi mbalimbali kama barabara, Umeme, Maji, Afya na elimu, huku ikiwawezesha wananchi kupata elimu bure, dawa katika vituo vya afya na umeme, ambao kwa sasa unafika mpaka vijijini kwa maana ya maendeleo ni watu.
Aidha Dkt Abbasi alieleza kuwa kauli mbiu ya Nguvu ya pamoja kutoka Clouds Media ni moja ya njia kubwa katika kutimiza malengo la wananchi kwa kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ambayo ndiyo inawawezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo.
Kwa upande wa sekta ya habari Dkt.Abbasi alieleza kuwa Serikali inafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na sekta binafsi katika sekta hiyo muhimu pamoja na sekta zingine ambazo zinawezesha wananchi kujikwamua kimaendeleo.
“Serikali ndiyo mwezeshaji mkuu wa sekta mbalimbali, Sekta haiwezi kufanya kazi nchini bila Serikali kuiwezesha kwa hiyo katika dhana hiyo hiyo ya Nguvu ya pamoja Serikali inashiriki kwa nguvu zote”, Dkt Abbasi.
Dkt. Abbasi aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuheshimu uwepo wa sekta binafsi katika sekta ya habari kwani mpaka sasa imewezesha upatikanaji wa leseni kwenye majarida na mageti 202, Vituo vya Televisheni 35 na Redio 160.
Alieleza pia kuwa nguvu ya pamoja ni pamoja na watendaji wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi ili kuwawezesha kupata huduma mara moja pale inapohitajika kwa sababu watakuwa wanatenda jambo la kuwafanya wengi kupata ajira katika sekta hizo.
“Ukiangalia uanzishwaji wa viwanda ni lazima kuna mtendaji alijituma kutoa leseni, maendeleo ya biashara mbalimbali, kilimo na sekta zingine ni lazima upate leseni ni hata kwenye sekta ya habari hii inamaana kuwa mtendaji wa Serikali unapoharakisha kwa kufuata sheria na taratibu kuhakikisha mtu anapata leseni ya kuanzisha kiwanda, Biashara kubwa au gazeti utakuwa umeajiri watu wengi bila kujua na hii ndiyo the power of man (Nguvu ya pamoja)”, Alisisitiza Dkt. Abbasi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu na Mumiliki wa Clouds media Group Joseph Kusaga aliahidi kushirikiana na Serikali katika kutangaza maendeleo ya nchi hasa kwenye sekta ya usafiri wa anga (shirika la ndege la Tanzania AirTanzania) pamoja na sekta ya utalii katika kampeni mbalimbali zitakazokuwa zinatangazwa Clouds Media.
Comments