Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewahakikishia wanafunzi 31,092 sawa na 47% ya watoto 64,861 ambao walifaulu katika mkoa huo kuendelea na masomo yao ya kidato cha kwanza kwakuwa serikali imeanza ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa 622 ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakaeachwa kwa kigezo cha uhaba wa madarasa.
RC Makonda amesema ongezeko la wanafunzi na ufaulu ni matokeo ya mafanikio ya Rais Dkt. Magufuli kutenga fedha zaidi ya bilioni 29 kwaajili ya elimu Bure ambapo kati ya hizo Bilioni 17.46 zinaenda kwenye elimu ya sekondari na tayari Serikali imejipanga na kuhakikisha kuwa tangu January 07 shule zote 147 za sekondari zimefunguliwa hivyo kila mzazi ahakikishe anamuandikisha mtoto ili kuendelea na kidato cha Kwanza.
Aidha RC Makonda amesema katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba mkoa huo umekuwa kinara kwa kufaulisha wanafunzi 64,861 sawa na 92% ambapo kati ya hao Wanafunzi 31,092 walikosa vyumba vya madarasa jambo lililoilazimu serikali kupambana kuhakikisha kila aliefaulu anaendelea na masomo.
Hata hivyo RC Makonda amesema lengo la ujenzi wa madarasa hayo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anatumia fursa ya Elimu Bure iliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli ya kuhakikisha Mtoto wa maskini anasoma ili kujikwamua kiuchumi na mwisho wa siku Taifa liwe na wataalamu wa kutosha.
Pamoja na hayo RC Makonda amewaonya wanafunzi watakaokwepa kusoma watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Comments