WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezinduaChaneli ya Taifa ya Utalii iitwayo Tanzania Safari Channel na amewataka watu wote waliopewa dhamana ya kuiendesha wahakikishe wanazingatia viwango vya kimataifa katika vipindi watakavyokuwa wanaviandaa.
“Vipindi vyenu ni lazima vivutie kama vile tunavyoviangalia katika chaneli za wanyama za kimataifa kama vile National Geographic, Discovery, Travel na zingine ili lengo lililokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwake litime.”
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Desemba 15) wakati akizindua chaneli hiyo kwenye Ofisi za TBC, Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ambapo ametoa wito kwa Wizara zote zinazohusika na uanzishwaji wa Chaneli hiyo kuhakikisha zinailea wakati ikijijenga kujiendesha kibiashara.
Amesema Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizotenga moja ya tatu ya eneo lote la nchi kwa ajili ya uhifadhi, ambapo kuna tamaduni za makabila mbalimbali, ngoma za kuvutia, vyakula vya asili, sinema za maisha yetu na lugha adhimu ya Kiswahili.
“Hivyo, kwa kuanzishwa kwa chaneli hii inayotengeneza vipindi na kuonesha vivutio hivi ndani na nje ya Tanzania itasaidia watalii huko waliko kujua huu utajiri wetu na kuchagua kuja kutalii nchini. Ni matumaini yangu kuwa hii Tanzania Safari Channel ninayoizindua leo itaongeza thamani katika kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea Tanzania.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametaja faidazinazotokana na utalii ambazo ni pamoja na kuliingizia Taifa fedha za kigeni, ambapo kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 2.3 zimeingia kwa mwaka 2017. Fedha hizo ni sawa na sh. trilioni 5.04.
Pia sekta hiyo ya utalii inatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni 1.5 wanaojihusisha katika shughuli mbalimbali zikiwemo usafiri wa ndani kwa watalii, uongozaji watalii kwenye maeneo yenye vivutio, kuuza bidhaa kwa watalii kama vyakula, vinywaji, vinyago, nguo, zawadi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema licha ya mafanikio hayo, lakini hatupaswi kuridhika nayo kwani Tanzania inapokea watalii milioni 1.3 kwa mwaka wakati nchi kama Misri na Afrika Kusini hupokea zaidi ya watalii milioni 10.
“Lazima tujiulize, ni kwa nini sisi tulio na vivutio vingi kuanzia hifadhi maarufu ya Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Ruaha, Sadani (Hifadhi pekee iliyopakana na bahari), Zanzibar ambako kuna fukwe maridadi, malikale, maporomoko ya maji na vingine vingi na baadhi ya hivi vivutio vimewekwa katika kundi la maajabu ya Dunia tunapata watalii wachache.”
Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuhusu uboreshwaji wa bustani katika barabara inayotokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, ambapo amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isac Kamwelwe asimamie jambo hilo pamoja na matangazo yanayowekwa katika barabara hiyo yaoneshe vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Kadhalika uzinduzi huyo ni utekelezwaji wa maagizo ya Rais Dkt. John Magufuli aliyoyatoa Mei 16 mwaka jana alipotembea TBC kuwa, pamoja na mambo mengine aliwataka waangalie uwezekano wa kuanzisha chaneli itakayotangaza hifadhi na vivutio vya utalii nchini.
Pia Uzinduzi wa Chaneli hiyo ya utalii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 29 iliyoielekeza Serikali kuweka mkakati wa kimataifa wa utangazaji wa utalii ili kuwavutia watalii wengi zaidi na kufikia idadi ya 2,000,000 ifikapo mwaka 2020.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Khamis Kigwangala. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isac Kamwelwe pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Comments