KIKOSI cha Simba SC leo kinatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa Mavuso mjini Manzini, Eswatini, zamani Swaziland kuelekea mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Mbabane Swallows kesho jioni.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza Saa 9:30 kwa saa za huko na saa moja zaidi kwa saa za Afrika Mashariki na utachezeshwa na refa Nelson Emile Fred atakayesaidiwa na washika vibendera Hensley Danny Petrousse na Gerard Pool, wote wa Shelisheli.
Simba SC itakuwa na kazi nyepesi kesho ikihitaji hata sare kusogea mbele kwenye michuano hiyo baada ya ushindi wa mabao 4-1 kwenye mchezo wa kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Simba SC wakifanya mazoezi jana jioni mjini Manzini kujiandaa na mchezo wa kesho
Kocha wa Simba SC, Patrick Aussems akiwapa maelekezo wachezaji wake jana mjini Manzini
Ushindi huo uliotokana na mabao ya Nahodha John Bocco mawili na wageni, Mnyarwanda Meddie Kagere na Mzambia Clatous Chama unawapa mzigo wa kushinda 3-0 kesho Mbabane ndiyo wasonge mbele.
Jana kikosi cha Simba SC kilifanya mazoezi mepesi mjini humo baada ya kuwasili ili kuwaondolea uchovu wachezaji wake baada ya safari.
Tayari kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems amesema anatarajiwa mechi ya marudiano itakuwa ngumu Mbabane Swallows wakicheza kwao, lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kusonga mbele.
Comments