MAHAKAMA Kuu ya Dar es Salaam imetengua maamuzi ya Kamati za Maadili za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumfungia maisha kujihusisha na mchezo huo, aliyekuwa Makamu wa Rais, Michael Richard Wambura.
Uamuzi huo umetolewa leo katika mahakama hiyo na Jaji, Dk. Benhajji Masoud kufuatia kesi iliyofunguliwa na Wambura kupinga kufungiwa maisha na Kamati za Maadili za TFF.
Kwa uamuzi huo, Wambura anarejea katika madaraka yake ya Umakamu wa Rais wa TFF na Uenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM).
Maana yake, Athumani Nyamlani aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo sasa anapoteza wadhifa huo aliopewa baada ya kuwa Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji.
Katika kesi hiyo TFF, iliyo chini ya Rais Wallace Karia ilikuwa inawakilishwa Wakili David Ndosi, ambaye hata hivyo hakuonekana wakati wa hukumu. Nakala za hukumu zinatarajiwa kuwafikia TFF mapema Jumatatu.
Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtuhumu kwa makosa matatu.
Katika taarifa yake, TFF ilisema kwamba ilichukuwa hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013.
Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye Kamati hiyo kwa tuhuma za makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi barua na kushusha hadhi ya TFF.
Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF iliyodai baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura ilionekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
Comments