SERIKALI kupitia kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda imewakaribisha wafanyabiashara kununua korosho na kuzibangua.
Mbali na uamuzi huo, Waziri Kakunda amesema Serikali bado inaendelea kuingia mikataba na wabanguaji ili kupunguza mzigo wa korosho.
Kakunda ametoa kauli hiyo wakati taarifa ya timu ya pamoja ya wataalamu kuhusu hali ya utekelezaji wa operesheni korosho iliyotolewa Novemba 27 ikionyesha kuwa itachukua muda mrefu kubangua korosho za msimu huu.
Novemba 12, Rais John Magufuli alitangaza Serikali kununua korosho yote kutoka kwa wakulima msimu huu kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo.
Licha ya Waziri Kakunda kusema haina shida kwa ubanguaji kuchukua muda mrefu, amewataka wafanyabiashara wanaoweza kubangua wenyewe wakae meza moja na Serikali ili wauziwe korosho.
“Kama mtu anatokea popote iwe ndani au nje akasema mimi nataka ninunue korosho nikabangue mwenyewe, labda ana bei nzuri aje tuzungumze. Ije mvua, lije jua korosho ziko kwenye maghala, kuna tatizo hapo? Zitabanguliwa tu muda wowote,” alisema.
Alisema ubanguaji unaendelea baada ya Serikali kuingia mkataba na baadhi ya kampuni.
“Leo (juzi) ilikuwa niende kuzindua ubanguaji wa kule Mtwara, kwa hiyo siyo tumekaa tunasubiri wateja, tunaendelea kubangua.
“Sido (Shirika la Viwanda Vidogo) ambao ni wabanguaji wadogo, wameshabangua tani sita. Bado kuna viwanda tulikuwa tunaingia navyo mkataba, hadi jana (juzi) tumeingia mikataba minne na bado tutaingia mingine zaidi ya 12,” alisema.
Inaelezwa kuwa kuna jumla ya viwanda 23 vya kubangua korosho na ambavyo uwezo wake uliosimikwa sasa ni kubangua jumla ya tani 42,200. Hata hivyo, uwezo wa mashine kwa kiwanda kimoja ni tani 11,142 kwa mwaka sawa na asilimia 26 tu ya uwezo uliosimikwa wa viwanda hivyo.
Taarifa hiyo ya timu ya pamoja ya wataalamu inaonyesha matarajio ya uvunaji wa korosho kwa msimu wa mwaka 2018/19 kufikia jumla ya tani 275,191 na kama viwanda vinane vinavyofanyakazi vingebangua korosho kwa kiwango kinachotakiwa cha tani 127,200 kwa mwaka, kazi hiyo itafanyika kwa miaka miwili.
Comments