Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameikabidhi timu ya soka ya African Sports “Wana kimanu manu fedha milioni 2.1 kwa ajili ya posho za wachezaji wa timu hiyo inayoshiriki Ligi daraja la pili Tanzania.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
Waziri, Mwalimu pia ameilipia timu hiyo shilingi laki tano (500,000) katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ‘TFF’ kwaajili ya Leseni za wachezaji na ada ya ushiriki wa timu hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo,Waziri Ummy amesema ameamua kutoa msaada huo ili kuiwezesha tmu hiyo kuweza kutimiza malengo yake ikiwemo kupanda daraja na kufikia hatua ya kucheza Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
“Kwani iwapo timu hiyo itarejea Ligi kuu soka Tanzania Bara itasaidia kukua kwa fursa mbalimbali za kiuchumi katika Jiji la Tanga.
“Sambamba na hilo lakini pia tumepokea mchango wa milioni tatu kutoka Kampuni ya GBP Oil ya Tanga ambao umeweza kuipa hamasa timu hiyo
kufanya vizuri katika mashindano inayowakabili.“Amesema Waziri Ummy.
Aidha pia Waziri Ummy aliitaka timu hiyo wahakikishe wanafanya vizuri katika michuano hiyo ili kuweza kurejesha hadhi yake ya miaka ya nyuma katika medani ya soka hapa nchini.
“Ndugu zangu wana African Sports msituangushe hakikisheni mnatumia misaada hii mnayoipata iweza kuwa chachu ya kufikia malengo yenu ya kufanya vizuri.“
Hata hivyo pia Waziri Ummy aliwafungulia akaunti ya fedha wachezaji wote wa timu hiyo katika benki ya NMB ili iwe rahisi posho zao kulipwa moja kwa moja kupitia benki ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.
Comments