Wanaharakati mbalimbali wa jiji la Dar es salaam ambao pia ni washiriki wa semina za jinsia na maendeleo(GDSS) wamekutana mapema wiki hii kujadili sera ya ardhi ya mwaka 2016.
Muwezeshaji wa semina ya GDSS wiki hii Bw. Kumbuka Mwakyusa kutoka shirika la Haki Ardhi akitoa elimu kwa wanaharakati kutoka kata mbalimbali za jiji la Dar es salaam |
Semina hiyo iliyoongozwa na wawezeshaji wawili kutoka taasisi ya watu binafsi ya Haki Ardhi akiwemo Kumbuka Mwakyusa na Vickness Dickson wakiwapa elimu wanaharakati hao tangu kuanza kwa mchakato huo mpaka kukamilika na mapungufu yanayopatikana katika sera hiyo.
Kwa mujibu wa wawezeshaji inaonyesha kuwa mfumo wa upatikanaji wa sera hiyo sio rafiki kwa wananchi wa hali ya chini kwani katika mchakato wa kutengeneza sera hiyo haukuwahusisha na badala yake wamechukua viongozi wakubwa wasiojua matatizo ya wananchi hao.
Bw. Kumbuka Mwakyusa akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika semina iliyofanyika mapema wiki hii makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP). |
Lakini pia mchakato huo haukukidhi matarajio ya wananchi wadogo kama wakulima, wafugaji, wavuvi nk. Kwani haukuwa shirikishi kama mchakato wa mwaka 1995 ambao ulijikita katika kuingia kijiji kimoja baada ya kingine kuchukua maoni ya wananchi.
Aidha wawezeshaji hao walisema kuwa mchakato huo ulifanyika kimya na kwa siri kiasi kwamba wananchi wengi hawakuwa na taarifa hivyo idadi ndogo sana ilipata nafasi ya kushiriki, lakini pia hao waliopata nafasi ya kushiriki maoni yao hayakuchukuliwa yote.
Mwanaharakati wa GDSS Bi. Subira Kibiga akichangia mada katika semina iliyofanyika mapema wiki hii makao makuu ya Mtandao wa Jinsia (TGNP). |
Lakini pia imeelezwa kuwa sera hii haikuwa na lengo zuri la kuwakomboa wananchi wadogo kwani imeeleza kuwa mwananchi anapohitaji mkopo anatakiwa kuweka rehani ardhi yake, na hii inahesabiwa ni kama njia ya kutaka kuwapokonya ardhi wananchi hawa pale wanaposhindwa kulipa deni.
Na jambo lingine ni kwa wananchi wa vijijini kulazimishwa kulipa kodi wakati toka zamani utaratibu huu haukuwepo kwa kuwa inafahamika wananchi wa vijijini hali zao ni duni, na wakigoma wanaambiwa hawajui umuhimu wa ardhi yao na kutishiwa kupokonywa.
Na pia sera hiyo imeipa mamlaka makubwa serikali ya kumiliki ardhi za vijiji na sio kama hapo mwanzo wananchi walimiliki ardhi yao kwa kupitia serikali zao za vijiji, na kudai kwamba viongozi wa vijiji hawana utaalamu wa kutosha hivyo kupewa kamishna kutoka serikalini aongoze zoezi hilo, lakini pia hii imeonekana kuwa itachochea mianya ya rushwa.
Kutokana na changamoto hizo zote wawezeshaji na wanaharakati walipitisha mapendekezo yafuatayo na kwanza ni kuondolewa mapango wa kodi kwa wananchi hao lakini pia kupewa elimu kupitia viongozi wao wa vijiji juu ya umiliki ardhi yao na mali asili.
Ndugu Abadallah Matata akitoa mchango wake katika semina ilikuwa ikijadili kuhusu mchakato wa sheria ya ardhi ya mwaka 2016. |
Lakini pia mikutano ya vijiji iwe na maamuzi juu ya ardhi yao na kupewa elimu juu usimamizi wa ardhi yao na kupunguziwa nguvu aliyopewa muwekezaji lakini pia kutopewa hati ya umiliki kwani atanyanyasa wananchi wa kijiji husika.
Sharia hii haijatoa ukomo kwa muwekezaji kuwa anatakiwa kumiliki kiasi gani cha ardhi hivyo wao wamependekeza asipewe zaidi ya ekari 200 kwa ardhi ya vijiji na kama atahitaji kwa vijiji tofauti basi zigawanywe ekali hizo lakini isizidi kiwango hicho na ikishindikana aombe kwenye ardhi ya jumla siyo ya kijiji tena.
Baadhi ya washiriki wa semina ya GDSS wakifuatilia kwa umakini semina hiyo |
Comments