Vita ya kumkomboa mwanamke inahitaji uelewa mpana wa mambo |
MCHANGO
wa wanawake katika maendeleo ya jamii tangu historia ya vizazi na
vizazi vilivyopita hauwezi kupuuzwa.Wanawake wamekuwa mstari wa mbele
katika kufanya shughuli za maendeleo, kuendesha familia na vikundi vya
kijamii, kulea watoto na kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli
mbalimbali za kiuchumi na kiutawala. Lakini pamoja na mchango wao ulio wazi kwa jamii nyingi, bado nafasi yao katika jamii ni finyu. Tena kadri ziku zinavyozidi kusonga mbele, nafasi yao katika michango ya maendeleo inaachwa nyuma au kupotoshwa kutokana na maslahi ya jamii, kikundi fulani au kuingia kwa upofu mkubwa miongoni mwa jamii pana. Historia inatuambia tangu enzi za wanafalsafa na wanazuoni wa mwanzo huko Ugiriki, wanawake hawakutambuliwa kama raia. Siku zote hawakuwa raia wa nchi hiyo na kwingineko. Hali ikaja kubadilika baadaye na sasa wanafurahia nafasi yao kama raia na kama ilivyo kwa binadamu wengine.Nchi ya Marekani pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kupigania demokrasia na haki za binadamu, imedumaza haki za wanawake kwa miaka mingi.Tangu kuanza kwa taifa hilo kubwa wanawake walikuwa hawaruhusiwi kupiga kura hadi miaka ya mwishoni mwa karne ya 19. Japo hili ni zuri sana, lakini historia hii inajaribu kupuuzwa na wanaharakati wengi hasa kutokana na ajenda ya kupigania haki za wanawake kuanzia nchi za Ulaya na Marekani.Ukweli wa historia ni kwamba, watu wa magharibi nao walichelewa kuzitii na kuzithamini haki za wanawake, ingawa kwa sasa wao wako mbele zaidi katika eneo hili ukilinganisha na Afrika na Asia. Mabadiliko katika eneo hilo yamekuja karne za hivi karibuni tu kutokana na kukua kwa maarifa, kuibuka kwa haki za binadamu na kubaini mchango wa wanawake kwa maendeleo ya harakati katika jamii.Bara la Afrika licha ya kutupiwa kila aina ya uchafu na lawama kutoka kwa wageni juu ya ukandamizaji wa wanawake, kwa karne nyingi bara hili limekuwa mstari wa mbele kuweka mbele haki za wanawake na kuwapa vipaumbele katika ushiriki wao kwenye maendeleo ya jamii. Tangu enzi za wahenga wetu, wanawake katika Afrika hawakubaguliwa katika kupiga kura au kuchagua viongozi au kuchaguliwa kuwa viongozi kama ilivyokuwa kwa nchi za Ulaya na Marekani kabla ya mabadiliko ya karne za hivi karibuni. Wanawake wa Afrika wameshiriki kikamilifu katika kushika nafasi za uongozi wa juu katika taasisi za kijadi katika maeneo mengi ya Afrika bila kupewa nafasi za upendeleo wala kusaidiwa na wanaume. Mifano iko mingi ya machifu na malkia wengi wanawake waliopata fursa za kuziongoza jamii za Afrika. Hapa Tanzania historia ya kila mkoa inahusisha wanawake, wapo kina Malkia Mgalula wa Ukimbu ambayo kwa sasa ni mkoa wa Tabora. Kina Wakalumwa kutoka huko huko na wengine wengi kutoka maeneo mengine. Bibi Titi Mohamed pia ni mfano mzuri wa wanawake waliokuwa mstari wa mbele katika uongozi. Pia kuna mifano ya wanawake wengi wa Kiafrika waliomiliki rasilimali kubwa na kufanya uzalishaji mkubwa bila kusaidiwa na kuingiliwa na wanaume. Mifano mingine ni ile ya wanawake wa Kiafrika walioshiriki katika harakati za kuzikomboa jamii zao enzi za ukoloni na uvamizi wa wageni. Ndani ya mgawanyo wa majukumu na kazi , wanawake wamechangia maendeleo kwa kiwango kikubwa kwa kufanya kazi nyingi na zenye manufaa kwa jamii nzima kwa miaka mingi sana. Tafiti nyingi zimebainisha ukweli huo ambao watu wa Magharibi na baadhi ya Waafrika wenyewe wanaupuuza kwa kudai kwamba jamii za Kiafrika zimewakandamiza wanawake kwa miaka mingi na hivyo kuwafanya washindwe kuwa wazalishaji. Mtazamo huo potofu uliojengwa hasa na wageni umesababisha kupindisha ukweli wa nini tatizo hasa la nafasi ya wanawake katika jamii, na kipi kifanyike ili kurudisha hadhi ya wanawake na kuwafanya wafurahie haki zao kama binadamu. Wanaharakati wengi wa sasa wanadhani ubaguzi wa wanawake unatokana na mifumo ya Kiafrika inayoweka mfumo dume mbele na kudumaza haki za wanawake. Hii si sahihi! Maana hata nchi za Ulaya, Asia na Marekani (ambako wanadai wamepevuka kwenye haki za wanawake), ni wanawake wangapi wameshika nafasi za juu za uongozi hadi leo? Au mifumo kama utandawazi na ubepari inayoweka nyuma nafasi ya wanawake imeanzia wapi? Je, siyo ukweli kwamba imeanzia na kuratibiwa huko huko Ulaya na Marekani ambako kampeni za wanawake zilianzia? Mfumo dume ni nadharia inayohitaji uelewa mpana ili kuukabili. Ajenda ya kutetea haki za wanawake inapaswa kutanguliwa na uelewa mpana wa vikwazo vya haki za wanawake, na ukweli wa nini chanzo cha kubinywa kwa haki za wanawake. Pia kuelewa faida za kuboresha haki za wanawake ndipo tutaweza kuweka juhudi hususan za kupigania haki za wanawake. Kuongozwa na kasumba na mahubiri ya wageni kamwe hatutotambua ukweli wa chanzo cha kubinywa kwa haki za wanawake. Bila kuichambua mifumo ya kisheria, ukoloni mkongwe na mamboleo, dini na tamaduni za kigeni, mwanamke wa Kiafrika hawezi kupata haki zake. Pamoja na sababu nyingine wanawake hasa wa Afika wamefika hapo walipo kutokana na kuingiliwa kwa tamaduni za kigeni zilizovuruga mfumo wa maisha ya Waafrika na kuigiza mifumo migumu ya kibaguzi na kandamizi inayodhalilisha wanawake. Kwa mfano, ujio wa dini za kigeni ambazo hadi leo zipo barani Afrika, ziliambatana na ubaguzi wa wanawake kutokana na mila na tamaduni zao. Mathalani, wageni kutoka Mashariki ya kati walikuja na mila za kuwafungia ndani wake zao na kuwatumia wanawake kama chombo cha starehe na kuwakataza hata kufika baadhi ya maeneo na kushika baadhi ya nyadhifa. Aidha wageni kutoka Ulaya nao walikuwa na mila zao na mifumo ya uongozi ya kuwabagua wanawake na kuwatumia kama chombo cha starehe. Chanzo ni Gazeti la Mwanachi. |
Comments