KATIKA toleo Na. 215 la Raia Mwema, Jenerali
Ulimwengu alitaja moja ya mapungufu ya watawala wetu Tanzania kwamba ni
ile hulka yao ya kutotaka kujifunza na kuiga kutoka kwa wenzetu wa nje
(Ughaibuni) wanaofanya vizuri. Aliandika hivi:
“Watawala wetu ni watu wanaosafiri mno, hadi wamesababisha malalamiko kwamba hawatulii nyumbani jinsi walivyo ‘kiguru na njia’. Inashangaza kwamba wanakwenda Ughaibuni kila uchao lakini hawana wanachojifunza huko kuhusu jinsi wenzao walivyopiga hatua za haraka kujiletea maendeleo na kuzikwamua nchi zao kutoka kwenye mateso ya umasikini.
“Wanakwenda Ughaibuni kushangaa maendeleo ya wenzetu na kufanya ‘shopping’ za upuuzi wakati nchi yao inadidimia. Hawana uwezo hata wa kutazama, kuona, kuelewa na kutaka kuiga kilicho kizuri.”
Hivyo ndivyo alivyoandika Jenerali katika toleo hilo. Napenda
kuuendeleza kidogo mjadala huo, na nianze kwa kuongeza kwamba; hata
kile ambacho kipo chini ya uwezo wa nchi yetu kukitekeleza wenyewe
wanachokiona huko Ughaibuni, hawawezi kukiiga.
Kwa mfano, watawala wetu kadhaa wametembelea miji ya wenzetu kama New Delji (Green Delhi)
wa India na Durban wa Afrika Kusini na wamejionea wenyewe jinsi ilivyo
misafi na ya kijani lakini wameshindwa kuiga. Wameshindwa kuligeuza
jiji letu la Dar es Salaam lifanane angalu kidogo na miji hiyo kwa
usafi na u-kijani.
Je; hivi kweli hata usafi wa jiji letu la Dar es Salaam na kuligeuza
kuwa la kijani, ni kitu kinachopaswa kusubiri ufadhili wa Wazungu? Kama
hivyo ndivyo, ni nini basi tunachoweza kumudu kukifanya sisi wenyewe
kwa pesa zetu wenyewe na kwa mikono yetu wenyewe?
Lakini kinachokatisha tamaa zaidi kutoka kwa watawala wetu hawa wa
zama hizi, ni kwamba wanashindwa kuiga hata kile chema kinachofanywa na
majirani zetu. Mfano mzuri ni hiki kinachofanywa kila mwaka na wenzetu
wa Rwanda kinachoitwa Umushyikirano.
Kwa miaka tisa mfululizo, Rais Paul Kagame amekuwa akiitisha, kila mwaka, mkutano wa kitaifa wa kujadili Muafaka wa Taifa (National Dialogue) – mkutano ambao umepachikwa jina la Umushyikirano.
Kila mwishoni mwa mwaka (Desemba 14 na 15) viongozi wa serikali kuu,
viongozi wa serikali za mitaa, wawakilishi wa vikundi vya jumuiya za
kiraia (NGOs), viongozi wa dini, wabunge, wanadiplomasia,
wafanyabiashara, Wanyarwanda wanaoishi Ughaibuni na wananchi wa
kawaida, hukutana kwa siku mbili kwenye ukumbi wa bunge kujadiliana
utendaji kazi wa serikali ulivyokuwa kwa mwaka huo na kupeana mikakati
kwa mwaka mpya unaofuata.
Ni katika mikutano hiyo ya Umushyikirano ambako miafaka ya kitaifa hufikiwa katika masuala mbalimbali nyeti yanayoigusa nchi. Kwa ufupi, Umushyikirano ni mikutano ya kila mwaka inayojadili mustakabali wa taifa la Rwanda.
Nimekuwa nikiifuatilia mikutano hii kwa miaka mitatu iliyopita
ukiwemo wa wiki iliyopita, na lazima nikiri kwamba imenisisimua. Kwangu
mimi, ni moja ya vitu vyema vilivyobuniwa na Rais Paul Kagame ambavyo
kama vitaendelezwa, vitaiwezesha nchi hiyo kupiga kasi ya maendeleo
kuliko tunayoishuhudia sasa.
Kinachonisisimua zaidi kuhusu Umushyikirano ni namna mikutano hiyo inavyoendeshwa. Inaendeshwa kwa uwazi mkubwa. Mbali ya mikutano hiyo kuwa live kwenye televisheni na redio, mijadala yake pia huwekwa kwenye tovuti.
Isitoshe, hata wale Wanyarwanda ambao hawakubahatika kuhudhuria
wenyewe mikutano hiyo mjini Kigali, hupewa fursa ya kuchangia maoni yao
au hata kuuliza maswali kupitia njia za simu za moja kwa moja na hata
kwa njia za sms na twitter.
Kwa uelewa wangu (naomba kusahihishwa kama nakosea), hakuna nchi yoyote ya Kiafrika yenye mkutano wa kila mwaka wa National Dialogue wenye ushiriki mpana na unaoendeshwa kwa uwazi kama huo wa Rwanda.
Na bado wako watu wanaomwita Rais Kagame “dikteta mkubwa” (mimi nasema kama ni dikteta, basi, ni ‘dikteta poa’ – benevolent dictator).
Japo wanakiri kwamba Kagame ameiletea Rwanda maendeleo ya kasi, haraka haraka wanaongeza:“lakini anabana uhuru wa kujieleza na ni mvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.”
Mimi sidhani kama kuna dikteta mkubwa popote pale duniani
anayeitisha mikutano ya mijadala ya kitaifa mithili ya huu wa kila
mwishoni mwa mwaka wa Rais Kagame unaoitwa Umushyikirano
ambao kila mwananchi ana haki ya kutema cheche zake, kuuliza lolote au
kuchangia lolote! Kama yupo dikteta wa namna hiyo, niambieni ni nani na
ni wa nchi gani.
Kwa sababu ya uwazi huo wa mikutano hiyo ya Kagame ya Umushyikirano,
hata mimi niliye Dar es Salaam (na ambaye si Mnyarwanda) nimeweza
kuifuatilia kwa miaka mitatu iliyopita, na naweza kuwa shuhuda wa
baadhi ya matunda ya mikutano hiyo.
Kwa mfano, katika mkutano wa Desemba mwaka jana, washiriki wengi
ukumbini na hata waliopiga simu, waliishutumu Serikali ya Rais Kagame
kwa kushindwa kuifanikisha haraka kampeni ya ujenzi wa nyumba bora za
kuishi kote nchini.
Kwa hakika, mjadala wa mwaka jana ulitawaliwa na utekelezaji wa
programu hiyo ya serikali ya kujenga nyumba bora kwa wananchi na
kutokomeza nyumba za udongo (nyakatsi) kote nchini Rwanda.
Viongozi wa ngazi za chini walilaumiwa sana kwa kuvurunda programu hiyo. Baada ya majadiliano makubwa, mkutano huo wa Umushyikirano ulikubaliana kwamba watakaozembea kwenye programu hiyo kwa mwaka 2011 watawajibishwa.
Matokeo yake ni kwamba
katika mkutano wa mwaka huu, uliofanyika wiki iliyopita, shutuma zilikuwa chache. Washiriki wengi walieleza kuridhishwa na programu hiyo ya kuteketeza nyumba za udongo nchini humo kwa kujenga za kisasa. Wenyewe wanakiri kwamba programu hiyo sasa imefanikiwa kwa asilimia 98!
katika mkutano wa mwaka huu, uliofanyika wiki iliyopita, shutuma zilikuwa chache. Washiriki wengi walieleza kuridhishwa na programu hiyo ya kuteketeza nyumba za udongo nchini humo kwa kujenga za kisasa. Wenyewe wanakiri kwamba programu hiyo sasa imefanikiwa kwa asilimia 98!
Hiyo maana yake ni nini? Hiyo maana yake ni kwamba muda si mrefu nyumba za udongo katika Rwanda zitakuwa ni historia.
Hebu tulitafakari jambo hili kwa undani kidogo. Ni hivi; wenzetu Rwanda, kwa kupitia mkutano huo wa Umushyikirano, walifikia mwafaka wa kitaifa kwamba nyumba za udongo (nyakatsi) katika Rwanda ziwe historia ndani ya miaka mitano.
Baada ya mwafaka huo wa kitaifa, wote wakaanza kuchapakazi kwa
pamoja kuitimiza ndoto hiyo, na kila mwaka wamekuwa wakikutana (kupitia
Umushyikirano) kufanya tathmini. Wamesutana na kunyoosheana vidole kwa wale waliovurunda lakini pia wamepongezana na kutiana moyo kwa wale waliofanya vizuri.
Matokeo yake ni kwamba mafanikio kwa mwaka huu wa 2011 unaoelekea
ukingoni, yamekuwa asilimia 98! Hiyo maana yake ni kwamba, muda si
mrefu nyumba za udongo za nyakatsi zitakuwa historia katika Rwanda.
Je; ni lini nasi nyumba za udongo katika Tanzania zitakuwa
historia? Si tu kwamba hatuna programu ya kuzitokomeza hapa nchini,
lakini hata wazo tu la kuwanayo programu ya namna hiyo halipo!
Najua wapo watakaodai kwamba Rwanda ni ka-nchi kadogo kenye watu
wachache, na hivyo ni rahisi kutekeleza programu ya namna hiyo. Hiyo ni
kweli – Rwanda ni ka-nchi kadogo kenye watu wachache ikilinganishwa na
Tanzania, lakini pia ni kweli kwamba ka-nchi hako kadogo hakana utajiri
mkubwa wa maliasili ambao Tanzania imejaliwa nao.
Kwa maneno mengine; kama tungekuwa na viongozi wa aina ya Kagame,
hakika tungeweza kuutumia utajiri huo mkubwa wa maliasili tulionao
kutokomeza zile tembe za Wagogo kule Dodoma au za Wasukuma kule Shinyanga au hata zile nyumba za msonge kule Upareni!
Ndugu zangu, nimetoa mfano mmoja tu wa kutokomezwa nyumba za nyakatsi kama moja ya matunda ya mikutano hiyo ya Umushyikirano
ya mijadala ya kitaifa yenye lengo la kufikia miafaka ya kitaifa katika
masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Taifa la Rwanda, lakini
naamini ipo mifano mingi tu mingine ya mafanikio.
Tukirejea hapa nyumbani kwetu, je; hatuwezi nasi kuiga jambo hilo jema la Rwanda? Kama Umishyikirano imeisaidia Rwanda kuharakisha maendeleo yao, kwanini isitusaidie pia sisi?
Kwanini tusiianzishe mikutano ya namna hiyo na kuitafutia jina letu
ili nasi ituwezeshe kufikia miafaka ya kitaifa kuhusu masuala
mbalimbali ya maendeleo yetu?
Nauliza hivyo; maana, kwa hali ilivyo sasa hapa nchini mwetu, hatuna National Dialogue.
Siku zote tunasikiliza tu kutoka kwa watawala wetu na si kujadiliana
nao. Ni lini nasi watatusikiliza na kujadiliana nasi kuhusu mustakabali
wa Taifa letu?
Afadhali zama za Nyerere; kwani mara moja moja alikuwa akienda pale
UDSM, ukumbi wa Nkrumah, kukutana na wasomi wetu na kujadiliana nao
kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Siku hizi si tu
kwamba watawala wetu wanakwepa majadiliano ya moja kwa moja na wasomi,
lakini hata mikutano tu na waandishi wa habari wanaikwepa?
Siku hizi wakubwa wetu wakiwa na jambo zito la kitaifa, hawataki
mjadala au ushauri wa mtu yeyote nje ya dola. Watawaita wazee (wa CCM)
pale Diamond Jubilee au ukumbi wa PTA na kuwahutubia au kuwaeleza
msimamo wao (wa serikali yao) kuhusu jambo hilo.
Wazee hao wa CCM ‘wakishahutubiwa’, watapiga makofi na kushangilia;
hata kama hawakukielewa vyema hicho alichozungumza bwana mkubwa
kinachohusu mustakabali wa taifa letu sote.
Staili hii hovyo ya uongozi ni ile wanayoiita kwa kimombo “top down”;
yaani kila kitu kinatoka juu kwa wakubwa kwenda chini kwa wananchi. Kwa
maneno mengine, wa chini ni wapokeaji tu wa amri na maelekezo!
Nihitimishe safu yangu hivi: Watawala wetu wanajigamba kwamba katika miaka 50 ya Uhuru, wamethubutu. Kama kweli wanathubutu, nawasihi basi wathubutu pia kujifunza somo la Umushyikirano kutoka kwa jirani yetu, Rais Paul Kagame wa Rwanda. Binafsi, naamini ni somo maridadi linaloweza kutusaidia.
Kwangu mimi; mikutano ya kila mwaka kama hiyo ya Rwanda yenye
ushiriki mpana, na yenye kujadili na kufikia miafaka ya kitaifa kuhusu
masuala mbalimbali, ni matumizi mazuri ya fedha za walipakodi kuliko
mikutano ile ya Rais Kikwete kama ule wa Sullivan.Cnazo ni Raiamwema.
Comments