Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa
Said Meck Sadiq kuomboleza vifo vya watu 13 ambao wamepoteza maisha
katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo zimekuwa zinanyesha
tokea juzi, Jumanne, Desemba 20, 2011. Aidha, Rais Kikwete amempa pole
Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na uharibifu mkubwa wa nyumba, makazi na
mali nyingine za wananchi uliosababishwa na mvua hizo ambazo pia
zimesababisha uharibifu wa miundombinu. Rais Kikwete pia ameuelekeza
uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusaidiana na taasisi na vyombo
vyenye uzoefu wa maafa kushirikiana katika kuendelea kuokoa maisha ya
watu, kusaidia waliozingirwa na mafuriko na kuwahifadhi na kuwasaidia
wale wote waliopoteza nyumba na makazi kutokana na mafuriko hayo.
Katika
salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Sadiq: “Nimepokea kwa
masikitiko habari za vifo vya wenzetu 13 ilivyotokana na mafuriko
yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo sote tumeishuhudia katika Mkoa wa
Dar es Salaam tokea jana. Amesema: “Nakutumia wewe rambirambi zangu
kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako kwa familia, ndugu na jamaa
waliopoteza wapendwa wao katika balaa hili la mafuriko. Wajulishe kuwa
msiba wao ni msiba wangu, naelewa machungu yao na niko nao katika hali
ya sasa ya maombolezo. Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu wote.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Napenda pia kupitia kwako kutoa pole zangu nyingi kwa
wote walioumia ama kupoteza mali zao katika mafuriko haya. Wajulishe
kuwa moyo wangu uko nao wakati huu wa mazingira magumu. “Chini ya
usimamizi wako, ningependa kuona uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na
taasisi na vyombo vyenye ujuzi na uzoefu wa kupambana na majanga na
dharura za namna hii, kuhakikisha kuwa tunaendelea kuokoa watu ambao
badowamezingirwa na mafuriko, tunawapa matibabu wale walioumia katika
mafurikohayo, na tunawahifadhi na kuwapa huduma za kibinadamu wote
waliopoteza nyumba na makazi yao katika mafurikio hayo.”
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
DESEMBA 21, 2011
DAR ES SALAAM
Comments