Na Zahira Bilal Maelezo Zanzibar 22/12/2011
Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imetoa Mkono wa Pole kwa wale wote waliopatwa na
ajali na kupoteza jamaa zao kutokana na Maafa makubwa ya mafuriko
yaliyosababishwa na Mvua zinazoendelea kunyesha katika Jiji la Dar es
Salaam na maeneo mengine.
Katika
taarifa yake iliyotolewa leo na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa
niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema Zanzibar imeguswa na
msiba huo na kuwaombea majeruhi wa janga hilo wapone haraka na wale
waliopoteza ndugu na jamaa kuwa na moyo wa subra katika kipindi hiki
kigumu.
Aidha
taarifa hiyo inasema kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya
Zanzibar Mvua kubwa zitaendelea kunyesha katika maeneo ya Dar es Salaam
na maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba kwa muda wa siku
tatu zijazo.
Kutokana
na hali hiyo wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari kwa kusafisha
mitaro iliyoziba na kuondoka katika maeneo yanayotuama maji ili kuepuka
na maafa ambayo yanaweza kujitokeza
Pia
taarifa hiyo imewataka wananchi kufuata kanuni za afya ikiwemo
kuchemsha maji ya kunywa na kuweka usafi katika maeneo yao ili
kujihadhari na maradhi ya miripuko.
Kwa
upande wa watumiaji wa Bahari taarifa hiyo imewataka wananchi
kusikiliza utabiri wa hali ya hewa kabla ya kufanya shuguli zao za
baharini ikiwa ni pamoja na uvuvi na usafiri.
Mvua
zinazoendelea kunyesha zimesababisha vifo vya watu zaidi ya 13 na
kuharibu miundo mbinu pamoja na makaazi ya watu katika maeneo
mbalimbali ya Tanzania Bara hasa katika Jiji la Dar es Salaam.
MWISHO
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Comments