Jenerali Ulimwengu Ifuatayo ni sehemu ya pili ya maswali 50 ninayodhani tunatakiwa kujiuliza wakati tukiadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika. Maswali 25 ya kwanza yalikuwa katika toleo la wiki jana: Je, hii ni nchi yetu na nchi ya wana wetu na vizazi vitakavyokuja (bila mwisho), na je, sisi tuliopo leo ni watu wenye dhamana ya kuitunza, kuilinda, kuitetea na kuiendeleza kwa niaba ya vizazi hivyo, au sisi dhima yetu ni kuitumia, kuitafuna, kuila, kuikamua hadi tone la mwisho ili tunapoondoka duniani kusiwe kumebakia kitu? Ni kwa nini tunawachukia wanetu na wana wao kiasi hicho? Ni kwa nini tumeachia masuala ya kuendesha nchi yetu yawe ni miradi ya wajanja wachache, walaghai na mabarakala, na watu waadilifu wamejiweka kando, wamekata tamaa, na hatima ya nchi hii wamewasabilia mabazazi? Leo tunawashangaa wabunge kutaka kujiongezea posho; ni lipi la kutushangaza? Mbona hivyo ndivyo watawala wetu wamekuwa wakifanya wakati wote? Mbona hatukushangaa wakati wan...