Mwenyekiti
wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema
pamoja na kutoa maazimio manane kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni katika
Akaunti ya Tegeta Escrow, Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha
Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa
kuwa nazo zinahusika.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba
alitaja mambo manne aliyoyatilia shaka katika uamuzi huo wa Bunge,
akisema yalilenga kulindana.
Mambo
hayo ni msingi wa hukumu kwa watuhumiwa, wahusika wengine kutotajwa,
mwingiliano wa mamlaka ya mihimili ya dola na wizara hizo kuachwa.
"Naona
kama kulikuwa na namna fulani hivi ya kulindana. Uamuzi wa Bunge
ulifikiwa kutokana na msukumo wa wananchi wa kutaka kujua hatima ya
suala la escrow na IPTL, wahisani kusitisha msaada kwa sababu ya
uchotwaji huo wa fedha pamoja na siasa, hasa zinazolenga urais mwaka
2015."
Jaji
Warioba alisema katika ripoti ya CAG na PAC, wametaja ukiukwaji wa
malipo ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gain) na ushuru wa stempu
(stamp duty) na kuwa wanaohusika katika hilo ni Wizara ya Fedha na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na upande mwingine ni Wakala wa Usajili
wa Biashara na Leseni (Brela) ambao uko chini ya Wizara ya Viwanda na
Biashara.
Alisema
wanaotakiwa kuidhinisha ulipwaji wa kodi ni TRA, huku akihoji kitendo
cha ripoti hizo mbili kuonyesha hisa zimeuzwa kwa Sh6 milioni wakati
ilikuwa ni Dola 6 milioni, nyingine kuuzwa kwa Dola 300,000 za Marekani
wakati ilikuwa Sh20 milioni.
"Hapa
kuna ufisadi, maana hata kampuni iliyotajwa kuwa imesajiliwa Brela
inaonyesha katika ripoti kuwa wahusika walioisajili hawakuweka majina
yao, waliweka saini tu," alisema.
Alisema
uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara ya Nishati na Madini lakini hasara
iliyotajwa kuonekana inazihusu zaidi Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda.
"Kulikuwa
na mchezo wa siasa, kwamba baadhi walindwe na wengine waachwe. Taarifa
ya kamati imesema Kampuni ya PAP kwa kushirikiana na ofisa wa ngazi za
chini wa TRA walidanganya. Hivi suala la kudanganya linafanywa na
maofisa wa chini tu, kwani wa juu hawahusiki?"
Alisema
kama ilivyokuwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutakiwa kujiuzulu kwa
maelezo kuwa alikuwa akifahamu mlolongo wa wizi huo, hata Hazina
ilitakiwa kubanwa kwa sababu nayo ilikuwa ikifahamu suala hilo...
"Tumeambiwa kuna uchunguzi unafanyika. Jambo hili bado halijafikia
mwisho, iweje wengine waachwe wakati imeonekana wazi kuwa Serikali
imepata hasara?"
Waliopata mgawo
Jaji
Warioba alisema suala jingine lililokosa majibu ni kitendo cha watu
wanaodaiwa kupewa fedha na James Rugemalira kutajwa majina yao sambamba
na akaunti ya aliyewapa, lakini wale waliodaiwa kuchota fedha hizo
katika magunia hawakutajwa.
"Taarifa
inasema waliolipwa fedha kupitia Benki ya Stanbic walichukua fedha
kwenye magunia na mfuko, sasa mbona hawajatajwa? Hata ukichukua fedha
katika gunia lazima benki itabaki na kumbukumbu ya jina la aliyechukua.
Tusubiri uchunguzi zaidi, ila naona kama ni dalili za kulindana.
Msingi wa uamuzi
"Ili
Bunge lipate msingi wa kufanya uamuzi huo walisema fedha za escrow ni za
umma na wananchi wanaelewa fedha hizo ni za umma. Binafsi nadhani
katika hili Bunge halikutenda haki," alisema.
Alisema
Akaunti ya Tegeta Escrow ilianzishwa kwa sababu ya mvutano kati ya
Tanesco na IPTL ili kuweka fedha mpaka hapo mzozo huo utakapomalizika...
"IPTL imeendelea kutoa huduma na umma umepata umeme kutoka katika
kampuni hiyo na kulikuwa na malipo. Sasa kuja kumaliza tatizo lazima
fedha za escrow ndiyo zingetumika kulipia gharama zote katika kipindi
kile ambacho walikuwa hawajakubaliana.
"Kwa
maana hiyo huwezi kusema fedha hizo ni za umma. Zilikuwa ni za kumlipa
anayetoa huduma ambaye ni IPTL, sasa kwa kuwa hawakukubaliana juu ya
gharama, waliamua fedha zibaki mpaka tutakapokubaliana.
"Kama
fedha hizo zingekuwa za umma zingewekwa katika akaunti ya escrow kwa
misingi ipi? Tusubiri uchunguzi zaidi ili tujue za umma zilikuwa kiasi
gani na za watu binafsi zilikuwa kiasi gani."
Alisema kama kulikuwa na fedha za Serikali ni kodi ambayo haikuwekwa wazi.
"Hii
ambayo wameeleza kwamba Serikali imepoteza Sh8 bilioni, ni kodi
inayotokana na mauzo ya hisa, siyo gharama za uwekezaji. Ukiuza hisa
lazima ulipe kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu. Hiyo ndiyo
hasara wanayoisema na haihusiani na escrow kwa sababu hata kama escrow
isingekuwa na matatizo, ilikuwa lazima walipe na ni utaratibu wa
kawaida," alisema.
Chanzo:Mwananchi
Comments