Kampuni ya Azam Media Limited, leo imetangaza kuwa Tido Mhando
ameteuliwa kuwa kaimu-Mkurugenzi mtendaji, Uhai Production Ltd (UPL).
Tido, anaungana na Rhys Torrington ambaye ni Mkuregenzi Mtendaji Mkuu
wa Azam Media Ltd na mtangazaji huyo maarufu wa mpira zamani nchini,
Mhando ataanza majukumu yake mara moja, ikiwa jukumu lake kubwa ni
utengenezaji na uboreshaji wa vipindi vya kitanzania katika televisheni
na redioni.
Mhando mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 kwenye tasnia ya utangazaji
na Uandishi wa Habari, ni mtu anayejulikana na kuheshimika katika
tasnia hiyo ukanda wa Afrika Mashariki na Ulimwenguni kote.
Alianza kazi kama DJ Radio Tanzania na mnamo mwaka 1985 alijiunga na
BBC idhaa ya Kiswahili Nairobi kama mwandishi wa habari. Ukuwaji wake
ndani ya shirika ulimpelekea kuhamishiwa jijini London mwaka 1991 ambapo
aliteuliwa kuwa Mwafrika wa kwanza kuongoza idara ya Idhaa ya Kiswahili
BBC.
Baada ya kurejea Tanzania, Mhando ameshika nyadhifa mbali mbali za
juu zikiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TBC na hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa
Mwananchi Communication Ltd.
Akizungumzia uteuzi wake, Mhando amesema; “Ninayo furaha kubwa
kujiunga na Azam Media, pia na changamoto kubwa zilizopo mbele yetu
kuifanya kuwa kampuni pekee ya Televisheni na Redio yenye ubora katika
kutoa burudani hapa nchini (Tanzania) pia na ukanda wote wa Afrika,”.
Mhando ofisi zake zitakuwepo katika jengo la kisasa la Uhai
Production Tabata, Dar es salaam. UPL inajulikana kwa ubora wake katika
kurusha matangazo yake moja kwa moja kama vile, Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara pamoja na vipindi vingine maarufu kama Kwetu House na
Morning Trumpet.
Pia katika wiki zijazo UPL itazindua studio zake mpya zenye kiwango
cha kimataifa ambazo zitamuwezesha Mhando kuwa na uwezo mkubwa wa
kutengeneza vipindi mbali mbali vyenye viwango vya kimataifa
akishirikiana na watengenezaji wazawa.
Akizungumzia uteuzi huo, Muingereza Torrington amesema: “Tunayo
faraja kubwa kwa Tido kujiunga nasi wakati tunakaribia kutimiza mwaka
wetu wa kwanza tokea tuanze kutoa huduma, inanipa furaha kwamba Azam TV
imekuwa kwa kasi na kuwa wasambazaji wakuu na watoa huduma bora
satellite Pay Tv Tanzania,”.
“Kwa uzoefu wake nategemea Tido atachukuwa jukumu la kutupeleka
katika hatua nyingine ya mafanikio kibiashara kwa kutengeneza vipindi na
burudani mbali mbali kwajili ya wateja wetu Tanzania na kuvuka mipaka
yetu. Na mtakia kilala kheri katika majukumu yake mapya,” amesema.
Comments