Dodoma. Bunge la Katiba jana lilianza kujadili Rasimu ya Katiba kwa
misukosuko kwenye Kamati baada ya kuvamiwa na kundi la wanaharakati
waliokuwa na mabango wakidai hati halisi ya Muungano yenye saini za
Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume.
Mwenyekiti wa Kamati namba tatu ya Bunge
Maalumu la Katiba, Shamsi Vuai Nahodha akiongoza mjadala wa kikao cha
kamati hiyo mjini Dodoma jana. Kulia ni mjumbe wa kamati hiyo, Anne
Makinda. Picha na BMK
Msukosuko mwingine uliozikumba karibu kamati zote zinazoanza kujadili
rasimu hiyo kwa kuanzia sura mbili zinazohusu Muungano ā sura ya kwanza
na ya sita na kuzua malumbano, ni maana ya maneno dola, shirikisho,
muungano na nchi.
Wakati waandamanaji wenye mabango wakiishia mikononi mwa polisi, suala
la Muungano lilitulizwa kwa kuitwa wanasheria kutoa tafsiri sahihi kwa
kila neno.
Katika kamati zote, suala la muda wa kamati kujadili sura hizo mbili kwa
siku mbili kila moja pia liliibua mjadala mkali, hadi kuwalazimisha
baadhi ya wenyeviti wa kamati kuamua kumwandikia mwenyekiti wa Bunge,
Samuel Sitta kuomba muda uongezwe.
Hali hiyo imejitokeza Bunge hilo likiwa limeshakaa siku 40 kabla ya
kuingia katika mjadala rasmi, baada ya kupoteza muda mwingi katika
kutengeneza kanuni za uendeshaji wa chombo hicho.
Wanaharakati wavamia
Wakati kamati zikijiandaa kuanza mjadala, wanaharakati wawili walivamia
kwenye ukumbi wa Royal Village, wakiwa na mabango yenye maandishi
yanayowataka wajumbe kutetea maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya
Katiba.
Hata hivyo, watu hao baadaye waliondolewa kwenye eneo la hoteli hiyo na maofisa wa usalama majira ya saa 2:00 asubuhi.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati Namba 9, ambayo inafanya vikao vyake
kwenye hoteli hiyo, Kidawa Hamis alisema kuwa hali ni shwari kwenye
kamati yake na wajumbe wanaendelea kuchambua rasimu.
Katika kumbi zilizopo kwenye Hoteli ya St. Gasper, pia watu wawili
walikamatwa wakiwa na mabango yanayowataka wajumbe kutambua kwamba
katiba ni mali ya wananchi na si ya wanasiasa.
Hati ya Muungano
Katika makundi karibu yote, jana kuliibuka hoja juu ya Hati ya Muungano,
wajumbe wakitaka kabla ya kuanza mjadala ionyeshwe kwa kuwa ndio msingi
wa hoja.
Hata hivyo, habari za ndani ya kamati zinadai kuwa hati ambazo
zilipelekwa kama vielelezo katika makundi hayo, zilitiliwa shaka na
wajumbe baada ya kukosekana saini za waasisi hao wa Muungano na nakala
halisi.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Anna Kilango alikiri kuwapo mjadala mzito
juu ya Hati ya Muungano, lakini akasema kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman Masoud Othman alisaidia sana kulitafutia ufumbuzi.
āKatika kundi letu, tulikuwa na mwanasheria wa Zanzibar na baada ya
majadiliano alitueleza kuwa viambatanisho vya Hati ya Muungano vilivyopo
kwenye randama ya Jaji (Joseph) Warioba ni sahihi,ā alisema Kilango.
Alisema kuwa pia katika kundi lao, kulikuwa na utata juu ya maana ya
maneno dola, shirikisho, nchi na Muungano, hasa kwa wajumbe ambao si
wabunge.
Kilango alisema kutokana na utata huo, Kamati yake imeazimia kumuomba
Sitta kuwapatia mwanasheria ambaye atasaidia kuelimisha wajumbe maana ya
vyombo hivyo.
āKanuni ya 56 fasili ya saba, inatupa nafasi kuwasiliana na mwenyekiti
ili kupata mtaalamu ambaye atasaidia kuwaelimisha wajumbe,ā alisema.
Kuhusu ufinyu wa muda, Kilango alisema katika kamati yake suala hilo
lilijitokeza kwa kuwa hadi jana walikuwa wanajadili sura ya kwanza pekee
yenye ibara tano.
āSote tumebaini muda ni mfupi na nitawasiliana na mwenyekiti ili tuongezewe muda,ā alisema Kilango.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 1, Ummy Mwalimu pia alieleza tatizo la hati,
tafsiri ya maneno na muda kwamba ilikuwa ni changamoto kubwa.
āNi kweli kuna changamoto ambazo zimejitokeza za wajumbe kutaka hati ya
Muungano ambayo imesainiwa na waasisi na muda ni mfupi,ā alisema.
Hata hivyo, alisema jana jioni alitarajia kukutana na viongozi wa Bunge
ili kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya wajumbe ili kuwezesha kuendelea
vizuri na mjadala.
āLakini kimsingi tunakwenda vizuri, wajumbe wanabishana kwa hoja na hakuna vurugu hali ni shwari kabisa,ā alisema Mwalimu.
Katika makundi mengine, mijadala ilikwenda mbali zaidi na kupendekeza
kuongezwa ibara itakayoruhusu kuongeza nchi nyingine kwenye shirikisho.
Kwa kundi jingine, kulitokea malumbano baada ya mapendekezo ya mabadiliko ya rasimu, hoja ambayo ilipingwa.
Mnyika ataka hati ya Muungano
Wakati huo huo, mjumbe wa Bunge la Katiba, John Mnyika aliwasilisha
bungeni hoja binafsi ya kupatiwa nakala halisi ya Hati ya Muungano.
Alisema hati ambayo imesambazwa kwa wajumbe sio halisi na ni maudhui ya hati halisi, jambo ambalo sio sahihi kisheria.
āMpaka sasa takriban wiki moja tangu kuomba hati hii kwa barua ā¦sijapata
majibu, lakini sheria ya Muungano mwisho kuna jedwali la sheria ambalo
lina hati ambayo haina saini na uthibitisho,ā alisema.
Nimemuomba kupatiwa hati hiyo kwa kuzingatia kanuni ya 4 (6) ambacho
kinatoa haki kwa mjumbe kupatiwa taarifa au nyaraka ya kumuwezesha
kutekeleza majukumu yake.
āSasa tunajadili ibara ya kwanza kifungu cha kwanza, ambayo imeibua
mjadala mkali kwa umma juu ya muundo wa Muungano, lakini naamini ilikuwa
ni vyema tunapojadili hoja hii tuwe na hati halisi ya Muungano na sio
nakala,ā alisema Mnyika.
Watatu mbaroni
Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David Misime alithibitisha kukamatwa
kwa watu watatu kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko isivyo halali na kuwa
na mabango yenye lengo la kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Alisema watu hao walikamatwa jana saa 3:30 asubuhi Wilaya ya Dodoma Mjini.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni mkazi mmoja wa Kilimani anayeitwa
Augustino Pancras (60), Cosmas Katebeleza (44), Mkazi wa Kikuyu na Jotam
Tarukundo (35), Mkazi wa Chidachi.
Alisema mabango waliyokutwa nayo yalikuwa na ujumbe unaosomeka āwajumbe
msijivunie wingi wenu humo ndani, sisi wananchi tupo nje na ndiyo wengi
maoni yetu yaheshimiwe.ā
Kamanda Misime alisema watu hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika kulingana na ushahidi watafikishwa mahakamani.
Mussa Juma,Sharon Sauwa na Habel Chidawali
Chanzo: mwananchi.co.tz
Comments