Wilson Kipsang, wa Kenya akimaliza kama mshinda wa mbio za Marathon za London 2014
Kijiji
cha Iten nchini Kenya kilijitangazia kuwa "makazi bingwa wa mbio za
masafa marefu" kufuatia mazingira yaliyojionesha Jumapili kijijini hapo
kwenye mji mkuu wa kaunti ya Elgeyo Maraket kufuatia ushindi wa pili wa
Wilson Kiprotich Kipsang kwenye mbio ndefu zijulikanazo London Marathon
zilizofanyika jijini London , Uingereza.
Kipsang alivunja rekodi kwenye mbio za "London Marathon" kwa kukimbia kwa muda wa saa mbili, dakika nne na sekunde 27.
Aliibuka mshindi dakika chache baada
ya jirani yake kutoka kijiji hicho hicho cha Iten na mshindi wa mara
mbili duniani, Ednah Ngeringwony Kiplagat alishinda mbio za wanawake kwa
kutumia saa mbili dakika 20 na sekunde 21 huku akimshinda mwanamke
mwingine mkazi wa kijiji cha Iten, Florence Kiplagat.
Kipsang na Kiplagat wanaishi umbali wa
mita 700 kutoka kila moja katika eneo la Mindililwa katika kijiji cha
Iten na wote walipigiwa kura ya kuwa wanariadha bora zaidi kwa mwaka
2013 na taasisi kubwa duniani inayohusika na masuala ya wanariadha AIMS.
Wakati huo huo mke wa Rais Uhuru
Kenyatta, bibi Margaret Kenyatta alikimbia katika mbio za London
Marathon kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya taasisi yake
inayoitwa "Beyond Zero" ya kusaidia wananchi wa Kenya kupata huduma za
afya karibu na maeneo wanayoishi, ambayo inahamasisha watu kuchanga
fedha za kuweka zahanati 47 za muda kwa ajili ya kutoa huduma za afya.
Umati ulikuwa unaanza kuondoka kwenye
uwanja wa riadha mwendo wa saa 12 jioni kwa saa za London wakati habari
ziliposambaa kote London kwamba mke wa Rais Kenyatta amevuka kilomita 32
katika mbio za kilomita 42.195 akiwa miongoni mwa mashabiki 36,000 na
wanariadha wafadhili waliojitolea kusaidia taasisi yake kwa ajili ya
watu maskini.
CHANZO:VOA
Comments