Mjengwa
NINGELIKUWA
Mjumbe kwenye Bunge Maalumu la Katiba msimamo wangu ungelikuwa wa
dhahiri kwenye hoja ya Muungano na hata namna ya upigaji kura; kwamba
ningepigia kura Muundo wa Serikali Tatu, na hivyo uwepo wa Tanganyika,
na ningependelea upigaji kura kwenye masuala muhimu uwe wa SIRI.(Hudugu Ng'amilo)
Lakini,
kwa vile mimi ni muumini wa nchi yangu niliyozaliwa, hata kama wenye
mitazamo sawa na mimi tungeshindwa kwa wingi wa kura, basi, ningebaki na
misimamo yangu na hata kuendelea kuipigia debe kuwashawishi wengine,
lakini, ningefanya yote kuunga mkono kilichoamuliwa na wengi. Na hapa
ndipo ulipo msingi wa hoja yangu, kuwa Katiba ni Maridhiano.
Maana,
nimepata kuandika, kuwa MARIDHIANO ndio msingi wa UHALALI wa mchakato na
hata Katiba yenyewe. Na ndiyo maana ya ukomavu wa kisiasa na kiuongozi.
Nilifarijika
sana kuwaona na kuwasikia Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Vuai Ali Vuai
(CCM) na John Mnyika (CHADEMA). Waliongea maneno ya hekima na busara
sana. Wote hawa ndio waliounda Kamati ya Maridhiano juu ya suala la kura
ya Siri au Wazi.
Na kauli
za wajumbe hao niliowataja zilifunikwa na kawa lililofumwa kwa maneno
yenye hekima na busara kutoka kwa Askofu Donald Mtetemela
aliyewawakilisha viongozi wengine wa kidini waliokuwamo kwenye kikao cha
Kamati ya Mariadhiano.
Askofu
Mtetemela alisema; pamoja na tofauti zilizozijitokeza, pande mbili
zimekubaliana kuacha kung'ang'ania misimamo yao ili tusonge mbele katika
kutimiza lengo la kupata Katiba Mpya.
Hivyo,
inanisikitisha ninaposoma habari kuwa wanaharakati wa Jukwaa la Katiba
kuwa wanapanga kulivunja Bunge kwa vile limetafuna bilioni 80. Siioni
busara na hekima ya wao wanaharakati kufikia hitimisho hili huku
wakifahamu kuwa hapa tulipofikia ni moja ya hatua muhimu kwenye mchakato
na pengine harakati za Watanzania kupata Katiba iliyo bora kuliko ile
ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1984.
Sasa kama
wanaharakati wa Jukwaa la Katiba wanatumia muda na fedha kuandaa
maandamano ya nchi nzima kwa madhumuni ya kuvunja Bunge Maalumu la
Katiba, swali, ni ili iweje? Kuna haja ya wanaohusika na mipango hii
kujitafakari upya. Ningedhani wangetumia rasilimali walizonazo kwenye
kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya Rasimu ya Katiba na yaliyomo.
Kuwapa mwanga zaidi wananchi katika kuyaelewa wanayojadili wabunge wao.
Hii ni
nchi yetu sote. Na hili la Katiba ni mchakato. Tusiwe wepesi wa kukata
tamaa. Ni vema na ni busara tukaupa nafasi na kuendelea kuunga mkono
mchakato wa Katiba unaoendelea sasa.
Chanzo Raia mwema.
Comments