Uganda
imesema itaitisha tena mazungumzo ya upatanishi ya Burundi, kufuatia
machafuko yaliyoipeleka nchi hiyo ndogo kwenye kingo za vita na
kuulazimu Umoja wa Afrika kujitayarisha kutuma kikosi cha kuwalinda
raia.
Serikali
ya Burundi na pia kundi kubwa zaidi la upinzani wamekaribisha hatua ya
kuanzisha tena mazungumzo hayo. Siku ya Ijumaa, (18.12.2015) Umoja wa
Afrika ulisema unajiandaa kutuma kikosi cha wanajeshi 5,000 nchini
Burundi kuwalinda raia, ukitumia nguvu kwa mara ya kwanza kutuma
wanajeshi katika nchi mwanachama dhidi ya matakwa ya nchi hiyo.
Hali ya
wasiwasi umekuwa ikiongezeka nchini Burundi hasa tangu watu wenye silaha
walipovamia kambi za kijeshi katika mji mkuu Bujumbura wiki iliyopita,
na kuzusha hofu katika kanda hiyo ambako kumbukumbu za mauaji ya kimbari
ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda zingalipo.
Burundi
ilitumbukia katika mgogoro mwezi Aprili baada ya Rais Pierre Nkurunziza
kutangaza mipango ya kuwania muhula wa tatu madarakani. Umoja wa Mataifa
unasema watu wasiopungua 400 wameuawa tangu mwezi Aprili, wakati uamuzi
huo wa Nkurunziza ulipozusha maandamano na baadae jaribio la mapinduzi
lililoshindwa.
Serikali yasema iko tayari
Waziri wa
ulinzi wa Uganda Chrispus Kiyonga, aliuambia mkutano wa wandishi wa
habari mjini Kampala siku ya Jumamosi, kwamba hali ya usalama nchini
Burundi imekuwa ikidorora kila kukicha. "Tunadhani sasa ni wakati
muafaka na muhimu kuanzisha tena majadiliano," alisema Kiyonga.(P.T)
Kiyonga
alisema karibu makundi 14 yanayowakilisha matabaka mbalimbali ya jamii
ya Burundi, kikiwemo chama tawala, vyama vya upinzani na mashirika ya
kiraia yatahudhuria mazungumzo hayo.
Msemaji
wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba alisema serikali imekuwa
tayari wakati wote kufanya mazungumzo na ilikuwa inasubiri mwaliko. "Ni
mazungumzo ya Warundi na ni Warundi tu watakaoamua nini cha
kujadiliana," aliliambia shirika la habari la Reuters.
Nzobonariba
hata hivyo aliondoa uwezekano wa kuzungumza na yeyote ambaye serikali
inamchukulia kuwa mhusika katika jaribio la mapinduzi lililofeli.
"Linaweza kuwa tukio la kutuwezesha kuwakamata kwa sababu wanatafutwa na
vyombo vya sheria vya Burundi," alisema.
Mazungumzo kuanza Desemba 28
Pancrace
Cimpaye, msemaji wa muungano mkubwa zaidi wa upinzani nchini Burundi
unaojulikana kama CNARED, alikaribisha hatua ya Uganda kuitisha upya
mazungumzo ya amani, inagwa alisema mungano wake ulikuwa bado
haujapatiwa mwaliko.
"Kwetu
mazungumzo ni kati ya pande mbili kwenye mgogoro, na pande hizo mbili
zinazozozana ni Nkurunziza na serikali yake kwa upande mmoja, na CNARED
kwa upande mwingine," aliliambia shirika la Reuters.
Mazungumzo
hayo yataanza tena nchini Uganda Desemba 28, na baadae yatahamishiwa
mjini Arusha nchini Tanzania, yaliko makao makuu ya jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), ambayo Burundi ni mwanachama wake.
Mwezi
Julai jumuiya ya Afrika Mashariki ilimeteua Rais wa Uganda Yoweri Kaguta
Museveni kuwa mpatanishi wa mgogoro huo na mikutano ya awali ilifanyika
katika mji mkuu wa Burundi katika mwezi huo.
Hali yazidi kuwa mbaya
Katika
mapigano mabaya zaidi tangu jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwezi
Mei, waasi walizishambulia kambi za kijeshi katika mji mkuu wa Burundi;
Bujumbura wiki iliyopita, ambapo karibu watu 90 waliuawa.
Mashirika
ya kuteteta haki za binaadamu yameripoti kuwepo na makabiliano mabaya
kati ya waandamanaji na vikosi vya serikali, mashambulizi ya silaha na
kuwekwa vizuwizini wakosoaji wa serikali. Lakini serikali imepuuza
ripoti za ukiukaji wa haki za binaadamu.
Mamia ya
maelfu ya Warundi wameikimbia nchi hiyo kunusuru maisha yao tangu
ulipoibuka mgogoro huo mbaya zaidi kuikumba Burundi tangu ilipotoka
kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa na mwelekeo wa kikabila
mwaka 2005.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.
Mhariri. Caro Robi
Chanzo:DW
Comments