TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Dkt. Edward Hoseah kutokana na kutorishwa na namna
taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na
rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya
Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kufuatia kutenguliwa
kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu
wa TAKUKURU Bwana VALENTINO MLOWOLA kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU.
Balozi Sefue amebainisha kuwa, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo
baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa TAKUKURU chini ya Dkt.
Edward Hoseah hauwezi kuendana na kazi anayoitaka.
“Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni Bandarini
na Katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Hivyo Mheshimiwa Rais
amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa
katika eneo hilo kwa muda mrefu lakini kasi ya TAKUKURU kuchukua hatua
haiendani na kasi anayoitaka” amesisitiza Balozi Sefue
Katika hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli ameagiza
kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ambao walisafiri nje ya nchi
licha ya Rais Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa
umma.
Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia
Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari
kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Balozi Sefue amewataka watumishi wengine wa umma kutii agizo la Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kuonya
kuwa atakayekiuka atachukuliwa hatua kali.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
16 Desemba, 2015
Comments