Mwenyekiti wa kampuni ya Quality Group, Yusuf Manji amemwandikia
barua Rais John Magufuli kumuelezea mchakato wa zabuni aliyoshinda
kuendeleza ufukwe wa Coco maarufu kama Coco Beach uliopo Kinondoni.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo kwa vyombo vya habari jana
ilisema Manji aliandika barua hiyo Desemba 5 mwaka huu akimuelezea
kiongozi huyo wa nchi usahihi wa mchakato wa zabuni ya kuendeleza eneo
hilo akiwa ameambatisha majibu ya pendekezo la mradi huo kuwa lilitakiwa
kutekelezwa na kampuni tanzu ya QGL, Q Consult Ltd.
Alisema kampuni hiyo ilishinda zabuni kwa kufuata masharti na vigezo vilivyokuwa vimependekezwa na Manispaa ya Kinondoni.
Manji katika barua hiyo alionekana “kuisemelea” Manispaa hiyo kuwa
Januari 20 mwaka huu QCL aliiandika barua yenye kumbukumbu namba
QCL/KMC/01/15 ili kusuluhisha kesi hiyo iliyokuwa mahakamani kwa muda
mrefu, lakini Manispaa waliidharau.
Alisema hakuna kipengele katika pendekezo la QCL kinachohusisha
uuzaji wa ardhi wala kuzuia umma kufika kwenye ufukwe, na badala yake
ilitilia mkazo mandhari nzuri kwa shughuli za kijamii na burudani kwa
umma kama ilivyo katika muongozo uliotolewa na KMC na Sheria ya
Usimamizi wa Mazingira.
“Kwa dhumuni la kutoonyesha upendeleo, katika barua yangu kwa
Mheshimiwa (Rais Dk Magufuli), niliomba afanye uchunguzi binafsi chini
ya ofisi yake tukufu ambayo nitashirikiana nayo kikamilifu na
nitakubaliana na hukumu ya itakayotokana na taarifa sahihi na za haki,”
alisema Manji.
Chanzo: Mwananchi
Comments