Sweetbert Lukonge na Hans Mloli
WAKATI benchi la ufundi la timu ya Simba likiendelea
kuwafanyia tathimini baadhi ya wachezaji wake wa kimataifa wanaofanya
majaribio ya kutafuta nasafi ya kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao,
uongozi wa klabu hiyo unatarajia kushusha straika mpya kutoka nchini
Ghana.
Kwa jinsi mipango ilivyo, straika huyo anatarajiwa kutua nchi leo au
kesho na kwenda moja kwa moja mkoani Morogoro kuungana na kikosi cha
timu hiyo kilichojichimbia huko kwa ajili ya maandalizi yake ya msimu
ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20, mwaka
huu.
Atakapofika huko, straika huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana
mpaka tunaenda mitamboni, atafanyiwa majaribio na Kocha Mkuu wa Simba,
Mcameroon, Joseph Omog ambaye anaendelea na harakati zake za kukisuka
upya kikosi hicho.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa ujio wa
straika huyo klabuni hapo umetokana na uongozi wa klabu hiyo kufanyiwa
mipango na baadhi ya maofisa wa timu ya soka ya Medeama ambao waliwaomba
wawatafutie mshambuliaji wakati walipokuwa hapa nchini na kikosi chao
kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya
Yanga.
“Ni kweli kabisa kesho au keshokutwa Jumanne tunaweza kumpokea
straika mpya kutoka Ghana ambaye anakuja kufanya majaribio na endapo
ataonyesha uwezo wa juu utakaomridhisha kocha basi tutamsajili.
“Straika huyo tumefanyiwa mipango na baadhi ya viongozi wa Medeama ya
Ghana ambao tuliwaomba watutafutie wakati walipokuwa hapa nchini na
kikosi chao kwa ajili ya kucheza na Yanga katika mchezo wa Kombe la
Shirikisho Afrika,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele ili azungumzie
suala hilo hakupatikana, lakini alipotafutwa makamu wa rais wa klabu
hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alipatika na alipoulizwa alionyesha
mshangao kisha akauliza: “Nani kakwambia jambo hilo, hakuna kitu kama
hicho, siku ile ya mechi ya tulikwenda kuwapongeza tu Medeama na hakuna
kitu kingine tulichozungumza nao lakini kama kuna lolote itajulikana.”Source Global Publishers
Comments