Arsenal wanahitaji kufanya usajili zaidi kutokana na kukosa wachezaji
wenye ubora wa juu huku Mesut Ozil, Alexis Sanchez na Granit Xhaka
wakisemwa kwamba si wazuri kwa kiwango hicho, hii ni kwa mujibu wa Stan
Collymore.
Arsene Wenger amemsajili Xhaka pekee kwenye dirisha hili la usajili
huku akisisitiza kwamba yuko tayari kutumia pesa kusajili isipokuwa kwa
wachezaji sahihi tu kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Arsenal tayari wamewakosa Jamie Vardy huku Gonzalo Higuain akitajwa
kuwa njiani kujiunga na Juventus, na hivyo basi, Collymore anahisi
kwamba kuna uhitaji mkubwa wa klabu hiyo kufanya usajili wa maana zaidi
ili kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa kwenye mbio za kuwania taji la ligi
la msimu ujao.
“Bado naamini kwamba timu hii ya Wenger itakuwa katika nafasi nne za
juu endapo tu watasajili beki wa kati mzuri na mshambuliaji wa kati
mzuri, vinginevyo sidhani kama watakuwa na fursa hiyo,” ameandika kwenye
gazeti la Sunday Mirror.
“Kwamba, kwa timu ambayo mawazo yake makubwa ni kupata nafasi ya
kushiriki Michuano ya Uefa kila msimu, hii litakuwa ni janga kubwa.
“Ni ukweli ulio wazi kwamba timu ya Wenger ina huo uhitaji, lakini
bado anaonekana kuwa mbishi kutumia fedha ambazo hata hivyo si zake,
unaweza kuona kwamba wakati wa Arsenal ya Sol Campbell, ukuta ulikuwa
hauoenyeki kirahisi.
“Vile vile bado sioni kama Mesut Ozil, Alexis Sanchez au Granit Xhaka
ni wachezaji wa viwango vya juu kiasi hicho. Kweli ni wachezaji wazuri.
Xhaka ni usajili sahihi, ni mchezaji ambaye ni katili uwanjani lakini
vile vile ananyumbulika.
“Lakini hata hivyo usajili huu hauna maana kwamba Arsenal ndio
wamemaliza kama ambavyowenzao wamemleta mtu kama Zlatan Ibrahimovic na
sasa mbioni kuleta mtu kama Paul Pogba.
“Kama Wenger angemleta Suarez wakati ule, sasa angekuwa anapiga goli
za kutisha kuliko hata anavyofanya kunako klabu ya Barcelona,”
amemaliza.
Comments