TWANGA PEPETA NA MSONDO KUMCHANGIA NGURUMO MATIBABU.
Bendi ya African Stars “Twanga Pepeta” imepanga kufanya onesho maalum kwa ajili ya kumchangia fedha za matibabu mwanamuziki mkongwe wa Bendi ya Msondo Ngoma Music Muhidin Ngurumo.
Onyesho hilo maalum linataraji kufanyika katika ukumbi wa Mango Garden uliopo Maeneo ya Kinondoni hapa Jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi tarehe 23-07-2011.
Burudani inataraji kutolewa na Twanga Pepeta yenyewe sambamba na Msondo Ngoma wenyewe na sehemu ya mapato ya onyesho hili yataenda kwa ajili ya kumchangia Mzee Ngurumo matibabu yake. Pia Kimwana wa Twanga Pepeta 2011 Mary Khamis anataraji kuonesha ustadi wake katika kusakata mitindo ya Twanga Pepeta.
Sehemu kubwa ya maandalizi yamekwisha kukamilika ili kufanikisha onyesho hilo na Twanga Pepeta itatumia onyesho hilo kwa ajili ya kutangaza albamu yake mpya inayotarajiwa kutambulishwa hapo baadae mwaka huu. Nyimbo zilizomo kwenye albamu mpya ya Twanga Pepeta ni pamoja na Kauli, Kiapo cha Mapenzi, Umenivika Umasikini, Mtoto wa Mwisho, Dunia Daraja na Penzi la Shemeji.
Twanga Pepeta imeamua kuandaa onesho hilo baada ya kuguswa na kutambua mchango mkubwa katika tasnia ya muziki alioutoa Mzee Ngurumo ikiwa ni pamoja na kuwa mshauri wa karibu wa Bendi ya Twanga Pepeta ambayo wakati ikikua alikuwa akiwafunda wanamuziki wa Twanga Pepeta kwa vipindi tofauti.
ASET inapenda kuwaomba wapenzi wa Muziki wa Dansi kuhudhuria kwa wingi katika onesho hili maalum ili kumchangia Mzee Ngurumo fedha za matibabu. Kwa kuingia kwenye onesho basi utakuwa umemchangia Mzee Ngurumo matibabu na kisha utapata burudani mbili kali toka kwa Msondo Ngoma, Twanga Pepeta na Kimwana wa Twanga Pepeta 2011 Mary Khamis.
Hassan Rehani.
Comments