KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye
----
Na Mwandishi Wetu-Dodoma
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema jitihada zake za kutetea matumizi mazuri ya raslimali za nchi hazitaendelea licha ya baadhi ya matajiri kupanga njama za kumchafua.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CCM mjini Dodoma leo, Nape alikanusha habari zilizoandikwa na gazeti la Mwanahalisi zenye kichwa cha habari : "Nape amgeukia Kikwete,ataka ajivue gamba"."Nimemini msimamo wangu umekuwa mwiba mkali kwa watu wengi, ambao baadhi yao wanaamini kuwa wanaweza kutumia fedha zao na nafasi zao kufanya wanavyotaka, nitaendelea kusimama imara kutetea matumizi bora ya raslimali ya nchi yangu," alisema.
Alisema vita dhidi yake vilianza pale alipoonyesha msimamo wake wa kupambana na ufisadi ambapo Aliwataka wana CCM na Watanzania kuyapuuza yaliyoandikwa katika gezti hilo ambayo amesema si kweli na hayana maana.Nape alisema mara zote penye ukweli uongo hujitenga na kuhoji kama hayo maneno aliyazungumza alipotembelea gazeti la Mtanzania, kwanini yasiandikwe huko na yakaandikwe na mwanahalisi ambao hawakuwepo.
Alibainisha kuwa lengo la ziara yake katika gazeti la Mtanzania ilikuwa ni kuweka uhusiano mzuri na vyombo vya habari nchini na hilo halikuwa gazeti la kwanza kulitembelea."Lengo lao ni kutaka kutugombanisha , wana CCM wapuuze kwani wanataka kuturudisha nyuma," alisema.
Alisema wakati anaanza mapambano dhidi ya ufisadi, baadhi ya watu walidhani ni nguvu za soda, lakini wameamua kujibu mashambulizi baada ya kuona wote waliokuwa kwenye mapambano hayo wana pumzi za kutosha.
Nape alisema kuwa ana taarifa kuwa mipango hiyo ni endelevu ambapo kundi la watu limepanga kuwavuruga baada ya kuona CCM hivi sasa inafanikiwa kurudisha imani yake kwa wananchi.
Alielezea kusikitishwa na habari hizo za nwana halisi ambazo zilimkariri Nape akisema Kikwenye ndiyo chanzo cha matatizo ndani ya chama ambapo hata walipompigia simu hivi karibuni na kumhoji aliwakatalia, lakini alishangaa wakaziandika.
Nape alisema hakuwa na mazungumzo ya siri alipofika Mtanzania kwani alikutana na wahariri na kuzungumza nao kama alivyofanya katika vyombo vingine vya habari.
Wakati huo huo habari zinasema kuwa mmoja wa vigogo wanaotuhumiwa na ufisadi na kutakiwa kujivua gamba ndani ya CCM amejiuzulu.Habari za kuaminika zinasema kuwa kiongozi huyo (jina tunalo) ameshatoa taarifa zake za kujiuzulu nafasi zake ndani ya Chama.
Hata hivyo Nape alipoulizwa kuhusiana na hilo hakutaka kuzungumza lolote.
Comments