WAZIRI wa Kilimo Japhet Hasunga amesema ipo haja ya
kuanzishwa kwa sheria ya kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto
zinzazoikabili sekta hiyo.
Hasunga aliyasema hayo hivi karibuni wakati
wa kikao cha siku moja baina ya wizara na watafiti wa kilimo kutoka Taasisi
mbalimbali za kilimo nchini.
“Kuna kila sababu yakuanzishwa
haraka sheria ya kilimo,kwasababu inayotumika sasa ni sera iliyotungwa 2013
ambayo pia inahitaji kupitiwa upya,” alisema
Hasunga aliongeza kuwa sheria
zinazotumika kwa sasa ni za bodi za mazao mbalimbali, ambazo pia zinachangamoto
zake na kuna mazao ambayo hayana bodi kiasi kwamba kuwatetea wakulima wa mazao
hayo inakua ngumu.
Mazao yaliyo katika utaratibu wa
bodi ni pamoja na zao la pamba, Kahawa, Chai, korosho, pareto na tumbaku kwa
upande wa mazao ya Biashara, mazao ambayo hayana bodi ni yale ya chakula ambayo
nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.
Hasunga aliwataka watafiti hao
kutumia kikao hicho kwakutoa maelezo yenye tija, nini kifanyike katika sekta ya
kilimo kwakuwa watafiti wana wigo mpana wakuweza kuitoa sekta hiyo kutoka
sehemu moja hadi nyingine.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Kilimo Omary Mgumba alisema kikao hicho ni cha kipekee kwakuwa kimewakutanisha
wataifiti na wataalamu kutoka taasisi za utafiti na watafiti wakufunzi wabobevu
kutoka vyuo vya kilimo nchini.
“Ni furaha kuwaona leo hii kwa wingi
wenu, eneo kubwa la kutiliwa mkazo ni katika suala la masoko, tunafanya tafiti
nyingi kuhusu mbegu bora lakini hatuna tafiti zakutosha kuhusu masoko ya mazao
ya kilimo,”alisema
Mtafiti kutoka chuo cha utafiti cha
Kilimo Naliendele Dk. Fortunus Kapinga , alisema kikao hicho kimekuja wakati
muafaka ambapo utafiti wenye tija na wenye kuzingatia wakati unahitajika zaidi
ili kutatua changamoto za kilimo nchini.
“Kazi yetu watafiti nikuhakikisha
utafiti wakina unafanyika ili kuondoa changamoto za wakulima, naamini
tutabadilishana uzoefu lakini pia tutaishauri serikali kuangazia katika tafiti
zaidi nakutujengea uwezo ili tuzalishe tafiti zenye tija na uzalishaji bora,
”alisema
Kikao kama hicho kitaendelea leo
baina ya wizara na wadau wakilimo wa sekta binafsi na baadaye kikao kama hicho
kitafanyika pamoja na wadau wa maendeleo ya kilimo wakimataifa na waliopo
nchini.
Baada ya vikao hivyo Wizara na wadau
wote wataamua mda gani sera ya kilimo ipitiwe upya nakuanzishwa mchakato wa
muswada wa sheria ya kilimo na hatimaye kupata sheria ya kilimo.
Comments