Skip to main content

Uongozi soko la Mabibo umesema unajitaidi kuboresha mazingira ikilinganishwa na hapo awali

Tokeo la picha la soko la Mabibo

UONGOZI wa soko la Mabibo maarufu mahakama ya ndizi umesema kuwa kwa sasa unajitaidi kuboresha mazingira ikilinganishwa na hapo awali kabla ya utawala mpya wa soko.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo Meneja Masoko wa soko hilo James Msulwa alisema kuwa limejiimarisha katika suala la usafi na usalama wa raia ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Amesema Soko hilo lipo chini ya uendeshaji wa serikali kwa sasa ambapo makusanyo ya maduhuri ya ushuri hukusanywa moja kwa moja na serikali nakuwasilishwa manispaa ya Kinondoni ushuru ni sh 500 hutozwa kila siku.

“Si vyema kujadili yaliyopita hususani uongozi uliopita isipokuwa ninachoweza kusema nidhamu ya ukusanyaji mapato kumechangia soko kuwa katika hali ya usafi na ubora,ukilinganisha na hapo awali,” amesema Msulwa.

Msulwa amesema soko la mabibo linajumla ya masoko 8 yaliyo gawanyika kwa mujibu wa vitengo vya mazao ya kilimo yanayouzwa sokoni hapo.

Fatuma Shabani ambaye ni mfanyabiashara wa nyanya soko namba moja(geti namba moja) aliliambia gazeti hili kuwa zipo kasoro ndogondogo ambapo zikifanyiwa marekebisho zitakwisha.

“Kero iliyopo hapa kubwa ni choo kutokana na wingi wa wafanyabiashara tuliopo ,geti namba moja peke yake lina wafanyabiashara zaidi ya 300,choo kina matundu 8 ya haja kubwa yakiwa mawili na haja ndogo yakiwa sita kwa jinsia zote mbili, unapofika wakati wakuelekea maliwato kunakuwa na mafuriko,” amesema

Akijibu suala la choo Msulwa alisema nikweli choo kina changamoto lakini wapo katika mchakato wakuboresha choo hicho kwa mazingira yaliyopo ili kikidhi mahitaji ya wafanyabiashara.

“Kama nilivyokuambia ndugu mwandishi soko hili lilikuwa chini ya uongozi mwingine na liligubikwa na mivutano ya maslahi ya hapa na pale kupelekea baadhi ya huduma kudhorota lakini usisahau kuwa lipo katika kipindi cha mpito kuwa kuna hati hati yakuhamishwa hapa kwa hiyo watupe subira”, amesema

Naye John Kimario alisema kuhusu usafi wa mazingira kwa maana uchafu aina ya taka ngumu huzolewa kila iitwapo leo mzabuni anajitahidi isipokuwa magari hayatoshi hivyo aliuomba uongozi wa soko kushughulikia suala hilo.

Msulwa amesema jambo hilo linashughulikiwa na saa chache kabla ya gazeti hili kufika sokoni hapo alikuwa katika mazungumzo na ofisa mazingira ili kuona uwezekano wa kuongeza gari za kuzoa taka.


Kuhusu vibaka na wazururaji sokoni hapo hutokea mara chache sana kutokana na ulinzi kuimarishwa baina ya kituo cha polisi jamii na wafanyabiashara sokoni hapo.

Comments