Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa (juu ya wastani) kwa baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam na Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Februari 14, 2019 kuhusu utabiri wa mvua za masika kwa mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, amesema kuwa, kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi chote kuanzia Machi mpaka Mei mwaka huu, maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka yanatarajia kuwa na mvua za wastani.
Hata hivyo, Dk. Kijazi amesema baadhi ya maeneo katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Kilimanjaro, Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga kuna uwezekano mkubwa wa kupata mvua kubwa (juu ya wastani).
“Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, tunategemea mvua hizi zitaanza wiki ya mwisho ya mwezi huu, ikianzia mikoa ya Kagera na baadaye kusambaa kwenye mikoa mingine ya ukanda huo,” amesema Kijazi na kuongeza.
“Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo mengi ya mikoa ya hii ya Kanda ya Ziwa, hata hivyo kwa baadhi ya maeneo machache ya Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Kibondo kutakuwa na upungufu wa mvua.“
Hata hivyo, amesema mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Zanzibar, Arusha, Manyara, Kilimanjaro na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, mvua za masika zinatarajiwa kuanza katikati ya wiki ya mwisho ya mwezi huu Februari.
Kijazi amesema ni vyema kwa mamlaka husika hasa katika sekta za kilimo, uvuvi, ujenzi na afya kuchukua tahadhari kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua.
“Kwa sekta ya kilimo, mikoa itakayopata mvua juu ya wastani ni vyema wakaangalia kulima mazao yanayostahimili unyevu nyevu mwingi kutokana mvua nyingi. Lakini pia kwa mamlaka ya miji, huduma za majisafi na majitaka zinaweza zikaathiriwa, ni vyema mifumo ya njia za kupitisha maji ikaimilishwa kuepuka mafuriko na athari nyingine,”
Mkurugenzi huyo amesema, TMA itaendelea kutoa mrejesho wa mvua katika utabiri wa siku 10 na siku tano watakaokuwa wakiutoa na kuwataka wananchi kufuatilia taarifa kwenye vyombo vya habari.
Mvua za masika zimekuwa zikisababisha mafuriko karibu kila mwaka kwenye maeneo ya mabondeni ambayo licha ya serikali kupiga marufuku watu kuweka makazi, bado yanaendelea kuwa na ujenzi holela.
Chanzo: Nipashe
Comments