MGOMBEA
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli,
amewataka Watanzania kuwa makini wasije kudanganywa na matapeli wa
kisiasa watakaokuja na ahadi za uongo.
Akizungumza
katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana, Dk Magufuli alisema
matapeli hao watakuja na ahadi nyingi, akawataka wananchi wawasikilize
na kuwapima kwa kauli na sifa zao kwa kuwa kuahidi ni rahisi kuliko
kutekeleza.
“Tusije
tukadanganywa na matapeli wa kisiasa, wakinamama mnafahamu matapeli wa
mjini walivyo na maneno matamu. Maendeleo ni changamoto na yataletwa na
sisi Wanamtwara,” alisema.
Miongoni
mwa matazamio ya Dk Magufuli ya Serikali atakayoiongoza kama
akichaguliwa kuwa rais, ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mtwara
kupitia Songea mpaka Mbambabay, baada ya kuboresha Bandari ya Mtwara na
kuwa ya kisasa kama ya Dar es Salaam.
Alisema
bandari itaboreshwa ili pia iongeze ajira kwa wakazi wa mji huo huku
mizigo ya nchi za Zambia na Malawi, ikipitia mkoani humo.
Aidha,
alisema Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza, itajielekeza zaidi
katika kukuza uchumi kwa watu. Akizungumza katika mikutano mikubwa na
midogo katika wilaya za Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini kuhusu zao
la korosho, Dk Magufuli alisema katika uongozi wake, lazima korosho
ilete uchumi mzuri kwa wakazi wa Mtwara.
“Mimi
shahada yangu ya tatu (PHD) nimesomea korosho. Hakuna anayeweza
kunidanganya. Korosho siyo tu tunda la ndani, bali hata ganda ni uchumi
kwa kuwa linatengeneza gundi na dawa ya kuzuia kutu,” alisema Dk
Magufuli.
Alisema
korosho ya Tanzania ni tofauti na korosho nyingine duniani, kwa kuwa
yenyewe huanza kuvunwa wakati maeneo mengine duniani wamemaliza kuvuna.
Kwa
mujibu wa Dk Magufuli, katika uongozi wake hataruhusu korosho kuuzwa
ghafi nje ya nchi, bali Serikali itahakikisha kunajengwa viwanda
vitakavyotumia malighafi ya korosho ili zao hilo lipande bei.
Kuhusu
tatizo la stakabadhi ghalani ambalo limekuwa likilalamikiwa na wakulima,
Dk Magufuli alisema wamuachie yeye atahakikisha kero ya mfumo huo
inaondoshwa na wakulima hawadhulumiwi haki yao.
Akiwa
Mtwara vijijini, alisema Tanzania imegundua gesi mkoani Mtwara, hivyo
akaahidi kuhakikisha gesi hiyo inaanza kunufaisha wakazi wa Mtwara kabla
ya kunufaisha wananchi wa mikoa mingine.
Katika
hilo, alisema atasimamia ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo,
ili vitoe ajira kwa vijana wa Mtwara, ambao watakuwa wamesoma katika
shule mbalimbali, ambazo kuanzia mwakani kutoka shule ya awali mpaka
kidato cha nne, itakuwa bure.
Awali
kabla ya kutoa ahadi hizo na zingine nyingi katika sekta mbalimbali,
Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM,
William Lukuvi, alisema Dk Magufuli ndiye mgombea pekee wa urais kwa
sasa aliyetembea kwa barabara umbali mrefu.
Kwa
mujibu wa Lukuvi, Dk Magufuli ambaye amemaliza awamu ya kwanza ya ziara
ya kampeni katika mikoa saba, kutoka Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya,
Njombe, Ruvuma na kumalizia Mtwara jana kwa barabara, pia ndiye
mgombeapekee wa urais aliyechaguliwa katika mchakato bora na ulio wazi.
“Wako
wanaodai kulikuwa na mizengwe wakati wa kumpata mgombea wa CCM. Ngoja
niwaambie, walikuwa wagombea 38, tukachuja mpaka wakabakia watano na
Magufuli akiwepo. Tukachuja tena katika mchakato wa wazi mpaka watatu na
Magufuli akawepo na wakati wa kumpata mmoja, ambaye ndiye Magufuli,
mchakato ulirushwa moja kwa moja na televisheni nchi nzima.“Sasa
tuwaulize wenzetu walikuwa wangapi na walimpataje huyo mgombea wao,
mbona hatukuwaona?” Alihoji na kuongeza kuwa Dk Magufuli ni mgombea safi
na hata marafiki zake si wa hovyo na watu wa hovyo wanaogopa
kumkaribia.
Lukuvi
alisema kama Watanzania wanataka bora rais, basi huyo si Dk Magufuli,
lakini kama wanataka rais bora, basi kati ya wagombea wote wa urais,
hakuna aliye bora kama Dk Magufuli.
Comments