CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) kimeeleza kutoshangazwa na matokeo ya utafiti wa
taasisi huru ya Twaweza yaliyotoa ushindi wa asilimia 65 kwa Mgombea
Urais wao, Dk John Magufuli, huku kikiahidi kuongeza kasi, nguvu na
mikakati zaidi katika nusu ya pili ya kampeni.
Hata
hivyo, kimeshangazwa na taharuki hasa kutoka miongoni mwa wasomi na
wanaharakati, kuhusu matokeo ya utafiti huo na kusema kilitegemea wasomi
na wanaharakati hao wangefurahia utamaduni wa tafiti za kisiasa
ulioanza kujitokeza nchini kwa vile unajenga.
Pia
kimesisitiza kuwa kimethibitisha kushiriki mdahalo wa wagombea urais
ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), lakini kikisitiza
uwashirikishe wagombea wenyewe na si wawakilishi wao, na pia wagombea
wote, hasa wa vyama vikuu wawepo na washiriki.
Juzi,
Taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo ya utafiti wake kuhusu ‘Sauti za
Wananchi’ kwenye siasa na kuonesha kuwa, kama uchaguzi huo ungefanyika
juzi, Dk Magufuli angeibuka mshindi wa asilimia 65 na Mgombea wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ambaye ana
asilimia 25.
Pia
Twaweza katika utafiti huo, ilisema wahojiwa hao walipoulizwa
wanajisikia kuwa karibu zaidi na chama gani, asilimia 62 walisema wako
karibu na CCM huku Chadema ikipata asilimia 25 na vyama vingine
vikiambulia asilimia zilizobaki.
Katika
utafiti huo uliofanywa mapema Agosti hadi Septemba mwanzoni mwaka huu,
wahojiwa waliulizwa swali ni mgombea yupi watampigia kura na kwa nini,
na majibu yalikuwa asilimia 26 walisema watampigia Magufuli kwa sababu
ni mchapakazi huku asilimia 12, walisema watampigia Lowassa kwa sababu
ya kutaka mabadiliko.
CCM haikushangazwa
Akizungumzia
matokeo hayo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ambaye
pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba alisema CCM
haikushangazwa na matokeo ya utafiti huo ambao umeibua mjadala mkubwa
miongoni mwa jamii wakiwamo wasomi na wanaharakati.
“Hatukushangazwa
na matokeo ya utafiti huu kwa sababu tano; moja; siku Ukawa walipomteua
Lowassa kuwa mgombea wao ndio siku CCM ilipohakikishiwa ushindi katika
uchaguzi wa mwaka huu.
CCM
hatukumteua kwa sababu tuliamini hakuna namna ambapo Watanzania wengi
watamchagua,” January aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam.
Aliitaja sababu ya pili kuwa CCM inafanya utafiti wa ndani wa kisayansi
kila wiki kujua mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo yanayohitaji
nguvu mahsusi na kwamba tangu utafiti huo uanze mwishoni mwa Agosti,
karibu kila wiki asilimia za ushindi wa CCM hazijawahi kushuka chini ya
asilimia 60 na zimekuwa zikipanda.
Tatu;
alisema kazi kubwa anayofanya mgombea wa CCM, Magufuli na Mgombea Mwenza
Samia Suluhu Hassan, kuzunguka nchi nzima kwa barabara na kuzungumza
moja kwa moja na wapiga kura inazaa matunda kutokana na kuwafikia wapiga
kura wengi, hasa wa vijijini, na wapiga kura wanawaelewa.
Aliitaja
sababu ya nne kuwa ni kutokana na kampeni kubwa zinazofanywa na wagombea
ubunge na udiwani wa CCM na makada na viongozi wa chama hicho katika
ngazi zote za nchi nzima kila siku kumuombea kura Magufuli, na kampeni
hizo kuzaa matunda.
Kuhusu
sababu ya tano, January alisema “Tunaamini pia migogoro ndani ya Ukawa
katika kipindi hiki cha uchaguzi iliyopelekea mitafaruku katika
kuachiana majimbo na baadaye, kutokana na uteuzi wa Mgombea Urais wa
Ukawa, kusababisha kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba na Dk Willbrod
Slaa, na migongano ndani ya NCCR- Mageuzi, ambayo yote yamepunguza imani
ya wananchi kwa vyama hivyo.”
Taharuki
ya wasomi Akizungumzia wasomi, January ambaye pia ni Mgombea Ubunge
Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, alisema CCM imeshangazwa na taharuki hasa
kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati kuhusu matokeo ya utafiti
huo.
“CCM
ilitegemea kwamba jamii ya wasomi na wanaharakati ingefurahia utamaduni
wa tafiti za kisiasa unaoanza kujitokeza hapa nchini ili siku zijazo
tujikite katika kurekebishana kwenye kanuni za utafiti na ithibati na
uhakiki wa ubora,” alieleza January na kutoa mfano wa utafiti wa
Sinovate mwaka 2010 ambao ulionesha kuwa Rais Jakaya Kikwete angeshinda
kwa asilimia 61, na kweli akapata asilimia 61.17 kushinda muhula wa pili
na wa mwisho.
“Tunasikitika
kwamba yanawekwa mazingira ya kutisha na kukatisha tamaa kwa watu
wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa nchini. Utafiti ni sayansi, na
matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti mwingine, si kwa
kuponda tu au kwa matusi na vitisho.
Ni vyema
tukajifunza kupokea habari ambayo haikufurahishi bila taharuki.” Kasi,
mikakati kuongezeka Akizungumzia mwenendo wa kampeni, January alisema
CCM inaridhika na mwenendo wa kampeni, na katika nusu ya pili ya kampeni
itaongeza kasi na msukumo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa mbinu
na mikakati mipya.
“Kwa
kifupi, mgombea Urais Magufuli na mgombea mwenza Samia, wanaendelea
vizuri na kampeni. Kila mmoja anafanya mikutano na wananchi kati ya
minane na 11 kwa siku na kukutana na maelfu kwa maelfu ya wananchi.
“Tunawashukuru
pia makada wa CCM wanaojitolea kwa hali na mali kukipigania Chama Cha
Mapinduzi na kumtafutia kura Ndugu Magufuli,” alisema. Midahalo ya
wagombea Kwa upande wa midahalo ya wagombea, alisema CCM imeshangazwa na
kauli ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kupitia kwa Katibu Mtendaji
wake, Kajubi Mukajanga kwamba CCM haijathibitisha kushiriki mdahalo.
Akifafanua
kilichotokea, January alisema; “CCM ilipokea mwaliko wa MCT na kuijibu
kwa barua ya tarehe 13 Septemba 2015 yenye kumbukumbu CCM/ OND/M/190/132
iliyosainiwa na Stephen Msami ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu,
ikithibitisha kushiriki mdahalo.”
Alisema
mbali ya hatua hiyo; CCM ilithibitisha kushiriki mdahalo huo kupitia
vikao mbalimbali na kwamba kauli ya Mukajanga inalenga kuwasaidia
kisiasa wale ambao hawajathibitisha au hawana nia ya kuthibitisha
kushiriki.
“Kwa
msingi huu, tunaamini ni vyema mdahalo huu ukaandaliwa na ushirika wa
taasisi mbalimbali zilizokuwa na nia ya kuandaa midahalo kama vile
UDASA, Twaweza na nyinginezo ili kuiondolea uwezo taasisi moja au
kikundi cha watu wachache, kuhodhi na kuwa na ukiritimba kwenye jambo
hili kubwa na muhimu.
“CCM
inapenda kusisitiza kwamba Magufuli amekubali kushiriki mdahalo wa
wagombea Urais, mdahalo uwashirikishe wagombea wenyewe na si wawakilishi
wao na wagombea wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki,”
alisema January.
ACT
yafarijika Kwa upande wake, Chama cha ACTWazalendo kimesema mbali ya
kuchelewa kutangaza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, lakini
kinafarijika kuwa chama pekee nje ya vyama vingine vya siasa kutajwa na
wapiga kura zaidi ya asilimia moja katika matokeo ya utafiti wa Twaweza.
Kimesema
kupitia utafiti huo, chama hicho kimeonekana kuwa cha nne katika
kukubalika kwa wapiga kura nyuma ya CCM, Chadema na CUF. Kadhalika
kimesema hadi sasa kimekusanya fedha Sh milioni 365 na kutumia Sh
milioni 363 huku kikiri kuwa na upinzani mkubwa katika majimbo 89
wakihitaji nguvu ya ziada.
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na Kampeni Taifa,
Nixon Tugara alisema katika utafiti wa Twaweza unaonesha kuwa chama
hicho hakikufanya vizuri na kwamba bado wana kazi kubwa ya kuwafikia
wapiga kura katika muda uliobakia wa kampeni.
“Licha ya
kuonesha hali hiyo, sisi ACT Wazalendo tunafarijika kwamba chama
kimekuwa chama pekee nje ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa kilichotajwa
na wapiga kura,” alisema Tugara.
Alisema
kutokana na kufanya vizuri katika kampeni na bidii kubwa ambayo mgombea
urais wa chama hicho na wagombea wengine wamekuwa wakifanya, wanaamini
kuwa utafiti ungefanyika leo wangefanya vizuri zaidi.
Tugara
alitoa mwito kwa wagombea wa chama hicho popote walipo kuchukulia
matokeo ya utafiti huo kama changamoto ya kuongeza bidii zaidi katika
kampeni zao. Kadhalika aliwahimiza wagombea na makampeni meneja na
viongozi wa chama kuwekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wananchi ambayo
katika utafiti huo yanaonekana bado kuunga mkono chama tawala.
Alitoa
mwito kwa taasisi nyingine kufanya tafiti nyingine kabla ya Uchaguzi
Mkuu kwa kuwa wanatambua utafiti ni moja ya maoni ya wananchi kuhusu
siasa, ingawaje hawawezi kubashiri hali itakavyokuwa siku ya uchaguzi.
Kuhusu
kampeni alisema tayari uongozi wa chama hicho umefika mikoa zaidi ya 10
na kuendelea kuwa na mtandao mpana hali ambayo ilisababisha kusimamisha
wagombea wengi zaidi ya vyama vingine ukiondoa CCM. Imeandikwa na Oscar
Mbuza na Lucy Lyatuu.CHANZO:HABARI LEO
Comments