Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless Lema amesema atamtoa kwa
mabavu bungeni Waziri wa nishati na madini,Profesa Sospetre Muhongo
katika kikao kijacho cha Bunge endapo atakuwa hajaondolewa kwenye nafasi
hiyo.
Mkakati huo wa Lema umeungwa mkono na Mbunge wa Arumeru Mashariki
(Chadema), Joshua Nassari ambaye pia amepanga kumtoa bungeni kwa nguvu,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge.
“Keshokutwa nakwenda bungeni kufanya kazi moja tu, nikimkuta Muhongo
bungeni ndipo nitafukuzwa ubunge moja kwa moja,” alisema Lema huku
akishangiliwa wananchi na kuongeza; “Nikimkuta Muhongo bungeni na Chenge
bado ni viongozi mimi nitakwenda kumshika Muhongo nimtoe bungeni kwa
sababu Katiba inaruhusu kila raia kukemea uovu.”
Profesa Muhongo na Chenge ni miongoni mwa viongozi ambao Bunge
liliazimia wawajibishwe na mamlaka zao kutokana na kashfa ya uchotwaji
mamilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Taifa, Desemba 22
mwaka jana kupitia wazee wa Dar es Salaam, alitangaza kumweka kiporo
Profesa Muhongo kwa siku mbili au tatu, ahadi ambayo haijatekelezwa.
Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
anayehusishwa na sakata hilo alishatangaza kujiuzulu na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akifutwa kazi.
Kauli ya Lema
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika Viwanja vya
Relini mjini Moshi, Lema alisema Januari 27 mwaka huu ataingia bungeni
akiwa na lengo moja tu la kumtoa kwa mabavu, Profesa Muhongo.
“Eti Tibaijuka kapewa tu bilioni moja kaondoka, waziri mwenye dhamana hajavuliwa nyadhifa. Rais Kikwete vipi?” alihoji.
Lema alidai kwamba sakata hilo, katibu binafsi wa Rais ambaye hata
hivyo hakumtaja kwa jina, ndiye aliyeandika barua kuruhusu fedha za
escrow zitoke lakini hadi sasa yuko salama na hajawajibishwa.
Pia, alihoji sababu za Jaji Werema kutofikishwa mahakamani wakati
ndiye aliyefanya makosa katika kutoa ushauri uliozaa sakata la escrow
badala yake watu wadogo ndiyo wanashtakiwa.
“Leo tunaona watu wanapelekwa mahakamani, Rais Kikwete nikuulize
swali, ulisema siyo fedha za Serikali ni za watu binafsi mbona mnashika
watu mnawapeleka mahakamani?” alihoji Lema.
Alisema Sh306 bilioni za escrow zingeweza kujenga nyumba 15,000 za
walimu, kununua mashine 300 za CT -Scan na kujenga barabara ya lami
yenye urefu wa kilomita 600 lakini zimeliwa na wachache.
Kauli ya Nassari
Akihutubia, Nassari alisema yupo bega kwa bega na Lema katika kumtoa
kwa nguvu bungeni Profesa Muhongo, huku akisema Bunge lijalo litawaka
moto.
“Lema umesema hapa ukimkuta Muhongo bungeni uko tayari kuvuliwa ubunge na mimi si mdogo wako? Tuko pamoja,” alisema na kuongeza:
“Nitamwambia Lema kaba kule na wewe Sugu (Joseph Mbilinyi, Mbunge wa
Mbeya Mjini) kaba kule halafu mimi narukia pale kwenye Siwa, tunaondoa
Siwa tutamfuata Muhongo alipo,” alisema.
Nassari aliwataka wananchi wa Moshi kufuatilia kikao hicho cha Bunge
na akisema haiwezekani maazimio ya Bunge yasitekelezwe kwa ukamilifu
wake na kwa wakati.
Chanzo: Mwananchi
Comments