Dar es
Salaam. Panga pangua ya saba ya Baraza la Mawaziri iliyofanyika juzi
imefikisha mawaziri 61 waliotemwa, kujiuzulu au kufariki dunia tangu
Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, huku mawaziri 16
wakihimili mawimbi hayo hadi sasa.
Katika
mabadiliko hayo saba yaliyofanywa katika kipindi cha miaka tisa, wako
waliobadilishwa wizara, kupandishwa kutoka naibu waziri kuwa waziri
kamili, huku sura mpya zikiingizwa.
Mabadiliko
hayo yalitokana na mawaziri kutakiwa kuwajibika kutokana na kashfa
mbalimbali, huku mengine yakitokana mawaziri kufariki na moja likitokana
na Waziri Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa.
Katika
panga pangua hiyo, mawaziri 16 wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo
tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark
Mwandosya, Stephen Wasira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli.
Wengine
ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia, Dk Mary
Nagu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kabla ya kuteuliwa kushika
nafasi hiyo, alikuwa naibu waziri na baadaye waziri wa Tamisemi.
Mawaziri
wengine waliopo sasa ambao mwaka 2005 walikuwa manaibu mawaziri ni
Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina Kombani, Christopher Chiza na
Mathias Chikawe.
Naibu
waziri pekee ambaye alikuwamo katika baraza la mawaziri la kwanza la
Rais Kikwete akiwa na wadhifa huohuo ni Dk Makongoro Mahanga ambaye sasa
ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.CHANZO:MWANANCHI
Comments