Wanafunzi 150 kati ya 1,000 waliojiunga na masomo katika Chuo Kikuu
Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) mwaka jana wamebainika kuwa na
ujauzito waliopewa na wenzao chuoni hapo.
Utafiti wa usawa na jinsia uliofanywa na chuo hicho kati ya Juni na
Novemba mwaka jana umebaini kuwa wanafunzi wanaopata ujauzito ni wale wa
mwaka wa kwanza.
Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa chuo
hicho, Dk Dativa Shilla katika warsha ya uchaguzi na uhusiano wa
kijinsia iliyofanyika chuoni hapo.
Alisema hali hiyo inatokana na kuwapo kwa vitendo vya ukatili,
manyanyaso na ubabe unaofanywa na wanachuo wa kiume dhidi ya wale wa
kike na hivyo kuwalaz imisha kufanya mapenzi bila hiyari yao.
“Kupitia utafiti huu tumeona hakuna usawa wa kijinsia wa kupata elimu
baina ya mwanamke na mwanamume kwa sababu mwenye ujauzito hawezi
kufanya vizuri katika masomo yake ukilinganisha na mhusika wa kiume,”
alisema.
Awali, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere, Amon Katunzi alisema ni wakati sasa kwa Serikali kutoa mikopo
kwa wanafunzi wote kwa sababu hatua hiyo itapunguza wanafunzi wa kike
kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi kwa sababu watakuwa na fedha za
kujikimu. “Lengo la warsha hii ni kutoa elimu na ushauri kwa wanafunzi
wa jinsi zote ili waweze kusoma vizuri na kuacha ushawishi wa
kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi. Pia, tunawashauri hata wale ambao
wapo katika ndoa wavumilie na kuepuka kupata ujauzito ili waweze kufanya
vizuri katika masomo yao,” alisema Katunzi.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho Gosbeth Kihanga ambaye
alikiri kuwapo kwa vishawishi chuoni hapo na kudai kuwa inachangiwa na
ugumu wa maisha hasa kwa wanafunzi wa kike.
Alisema kupitia kongamano hilo wamejifunza na kuelewa mengi hususani
katika suala la kupanga na kugawana majukumu, kubadilisha mtazamo na
kuacha kutumia ubabe katika uhusiano wa mapenzi.
Chanzo: Mwananchi
Comments