YANGA inatarajia kufanya maamuzi magumu ya kumchukua kocha Mecky Maxime
lakini mwenyewe ametangaza utamu kwamba akitua klabu hiyo itavuna vipaji
vingi kutoka katika jicho lake.
Akiongea na saluti5, mmoja wa vigogo wa Kamati ya usajili amesema katika
kikao cha awali na kocha huyo kijana mwenye mafanikio, amewaambia
kwamba endapo watakamilisha haraka mchakato wa kumchukua, Yanga
itanufaika na kazi yake ya kuvumbua vipaji.
Bosi huyo amesema Maxime amewahakikishia kwamba anajua wapi vinapatikana
vipaji bora ambapo Yanga itakuwa bora zaidi kwa kuwapatia wachezaji
wapya wenye uwezo zaidi ya Shiza Kichuya, Muzamir Yassin na Mohammed
Ibrahim “MO” wanaotamba Simba wakitoka katika uvumbuzi wake.
Aidha bosi huyo amesema ujio wa Maxime ndani ya Yanga utaambatana na
usajili wa mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuph ambaye nae
anatakiwa na kocha George Lwandamina.
“Tunamtaka kweli Maxime, unajua sisi tunataka kufanya maboresho makubwa
katika benchi letu na jicho letu limetua kwa Maxime na tulitaka
kumchukua mapema lakini tulisitisha mpango huo kwa muda,” alisema bosi
huyo.
“Tumekutana na Maxime mwenyewe, hana shida katika kutua hapa na
ametuambia kwamba anajua Yanga inayumba wapi katika kupata wachezaji
wazuri na akitua hapa kazi hiyo ataifanya yeye kwa kumuonyeshwa
Lwandamina wachezaji bora.
Comments