Frank Mvungi
MAELEZO
DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka wazalishaji na wajasiriamali nchini kuhakikisha kuwa bidhaa
wanazozalisha zinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa Leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya
Uhandisi wa Ujenzi ya Shirika la Viwango Nchini, Mhandisi Stephen Minja wakati wa
ziara ya waandishi wa habari kutembelea na kujionea namna maabara za shirika hilo
zinavyotekeleza jukumu lake la kuhakiki viwango vya ubora hapa nchini.
Akifafanua zaidi Minja amesema kuwa mabara za shirika hilo zipo kwa ajili ya
kuhudumia wazalishaji wa bidhaa mbalimbali na wale wanaoingiza bidhaa kutoka nje
ya nchi lengo ili kuhakiki ubora wa bidhaa zote ili kuepusha athari zinazoweza
kujitokeza kwa watumiaji.
“Maabara yetu ina viwango vya kimataifa na gharama zake ni nafuu ambazo kila
mwananchi anaweza kumudu lengo likiwa ni kutoa huduma kwa wananchi na
kuchangia kuchochea maendeleo kwa kudhibiti bidhaa hafifu” alisema Minja
Aliongeza kuwa maabara hiyo inapima bidhaa za ujenzi kama nondo, chokaa, vigae,
mbao, mabomba ya maji, simenti, nguzo za umeme,matofali,zege, mchanga na
bidhaa zote zinazotumika katika ujenzi wa barabara ikiwemo lami.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kitengo cha maabara ya umeme, Mhandisi Anectus
Ndunguru amesema kuwa vifaa vyote vya umeme vinavyozalishwa na kuingizwa nchini
lazima vipimwe ubora wake kuona kama vinakidhi vigezo ili kuepusha majanga.
Alitaja baadhi ya vifaa ambavyo lazima vihakikiwe ubora wake kuwa ni vifaa vyote
vinavyotumika katika kujenga mfumo wa umeme katika majengo, taa za majumbani,
pasi, redio, televisheni, waya .
Akizungumzia athari za kutumia vifaa visvyo na ubora Ndunguru amesema kuwa athari
za matumizi ya vifaa hivyo ni makubwa ikiwemo kusababisha majanga na kupotea kwa
umeme hivyo kuongeza gharama kwa mtumiaji.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa likisisitiza matumizi ya bidhaa zenye
ubora na zilizohakikiwa na kuepuka bidhaa hafifu ambazo kwa sasa zimedhibitiwa na
shirika hilo kwa kiwango kikubwa hali inayochochea ukuaji wa sekta ya Viwanda hapa
nchini.
Comments