Ngolo Kante ni jina linalozidi kukua siku hadi siku huku
akizidi kujizolea tuzo kutokana na kiwango bora anachokionesha tangu
ajiunge na klabu ya Chelsea.
Kante ambaye ameisaidia Chelsea kutwaa ubingwa msimu huu na hilo
likiwa kombe lake mara mbili mfululizo na timu tofauti, usiku wa jana
alijinyakulia tuzo mpya.
Kante amefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa waandishi
wa habari za soka, tuzo ambayo huandaliwa kila mwaka na waandishi wa
masuala ya soka nchini humo.
Tuzo hizo ambazo zilitolewa katika hotel ya Landmark nchini Uingereza
zilishuhudia Mfaransa huyo akiweka kabatini tuzo yake kubwa ya pili
ndani ya mwezi mmoja.
Kante ambaye msimu uliopita pia alifanikiwa kubeba kombe la Epl akiwa
na Leicester City ameweka wazi ugumu ambao wanaweza kukabiliana nao
katika msimu ujao wa ligi.
“Msimu ujao tutakuwa na changamoto mpya kwani ukiwa bingwa na huku
uko katika michuano mingi ni wazi kwamba unaweza kuwa na wakati mgumu
uwanjani” alisema Kante.
Tuzo hiyo ambayo mwanzoni ilikiwa ikishikiliwa na Eden Hazard, Kante
aliipata kwa kura nyingi baada ya kupigiwa kura nyingi na kumshinda
Hazard na Delle Ali wa Tottenham Hotspur.
Kante amesema anajisikia faraja sana kushinda tuzo hiyo na
anawashukuru wachezaji wenzake ambao bila wao asingeweza kuchukua tuzo
hiyo, Kante alinunuliwa na Chelsea kwa dau la £32m kutoka Leicester
City.
Comments