Na Baraka Mbolembole
Salum Telela ameshindwa kuzungumzia ‘mustakabali’ wake baada ya
kumaliza mkataba wake katika klabu ya Yanga SC. Nahodha huyo wa zamani
wa timu za Taifa za vijana na klabu ya Moro United ameshinda mataji
mengi katika misimu yake 6 akiwa na timu hiyo iliyomsaini akiwa kinda
mwaka 2010 akitokea Moro United.
Nilifanya naye mahojiano mafupi na kikubwa nilitaka kufahamu ni wapi
atacheza msimu ujao kufuatia kuwapo kwa habari kuwa anahitajika sana na
mahasimu wao Simba SC.
“Nimecheza kwa misimu 6 katika timu hii na nimepata mafanikio makubwa
ikiwemo ushindi wa mataji ya ligi kuu (2010/11, 2012/13, 2014/15,
2015/16,) nimeshinda Kagame Cup 2011 na 2012, Ngao ya Jamii 2013, 2014,
2015, pia taji moja la FA.”
“Msimu uliopita kulikuwa na ushindani mkubwa sana lakini niliweza
kupambana na kucheza zaidi ya michezo 20. Ukitazama hata uwiano wa mechi
kwa wachezaji wa nafasi yangu hazikupishana sana. Nilikuwa na msimu
mzuri. Pia nafurahi kufanya kazi na kocha mzuri kama Hans Van der Pluijm
na kila mmoja katika benchi la ufundi.”Nilimuuliza, Telela, ni kweli
unaondoka Yanga? lakini akajibu kwa namna ya kutohitaji kuzungumzia
mambo ya usajili. “Habari hizo naomba tuachane nazo, ni mapema kujadili
hayo.”
Telela amekuwa akiwindwa na Simba lakini Yanga wamepanga kukamilisha usajili wake kabla ya kumalizika kwa wiki hii.
Comments