Mkongwe katika anga la bongo fleva, mwanadada Judith Wambura a.k.a Lady Jay Dee amesema yuko tayari kufanya kazi na staa wa muziki huo Diamond Platnumz, endapo atahitaji lakini kinachoweza kukwamisha ni ratiba yake ya kazi.
Jay Dee amelazimika kutoa kauli hiyo kutokana na kuongezeka kwa minong'ono kuwa wawili hao wanakwepana, na hawataki kufanya kazi kwa pamoja, ambapo amekuwa akikabiliwa na mambo mengi kwenye ratiba yake.
Akiwa katika Kitengo ya Planet Bongo ya EATV, Jay amesema hana tatizo na msanii yoyote nchini na yuko wazi wakati wowote, lakini akasita kutaja ni wakati gani atafanya kazi na Diamond.
"Kwa sasa nina ratiba za mambo mengine, lakini akinihitaji niko tayari na tutafanya kazi wakati muafaka nikiwa na na nafasi" Alisema Jay Dee.
Mwezi Novemba mwaka jana, Diamond alipozungumza na EATV kuhusu suala hilo alisema yuko tayari kufanya kazi na mwanadada huyo, lakini tatizo ni kubanwa na ratiba ambayo imekuwa haimpi nafasi.
Kwa kauli hizo, sasa ni dhahiri kuwa wawili hao hawana shida kufanya kazi pamoja lakini huenda wanaogopana, huku kila mmoja akisubiri mwenzake amuanze, maana hadi sasa hakuna ambaye ameomba kufanya kazi na mwezake huku wote wawili wakidai kukwamishwa na ratiba ya kazi zao.
Comments